Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa
amewataka waandishi wa habari mkoani Tanga kuutangaza mkoa wao
kiutalii, pamoja na vivutio vyake na kuacha kuandika habari ambazo
hazina faida kwa jamii na Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
juzi wakati akielezea maendeleo ya Mkoa wa Tanga mwaka 2013/14, Gallawa
aliwataka waandishi wa mkoa huo kuitumia vyema kalamu yao kwa
kuvitangaza vivutio vilivyoko mkoani humo.
Alisema Mkoa wa Tanga una vivutio vingi vya
utalii, lakini vimekuwa havitambuliki ndani na nje ya nchi kutokana na
kutotangazwa katika vyombo vya habari na hivyo kuwa chanzo cha
maendeleo kudidimia na Serikali kukosa mapato.
“Nashangazwa kuona Tanga ina vivutio vingi vya
kiutali zikiwemo fukwe, mapango pamoja na mbuga ya wanyama, lakini sioni
watalii wa ndani wala wa nje wanaokuja---tuweni wazalendo tupate
maendeleo” alisema na kuongeza:
“Nadhani mko waandishi wa vyombo vyote hapa nchini
na natambua kuwa mko mahiri katika kuandika na msomaji kuvutika kwa
kile mnachokiandika,sasa kwanini hamuutangazi mkoa wenu kiutalii au
mmeghafirika,nawakumbusha” alisema Gallawa
Gallawa alisema Mkoa wa Tanga umejaliwa kuwa na
vivutio vingi vikiwemo mbuga ya wanyama ya Saadan, Mapango ya watu wa
kale yalioko Amboni pamoja na fukwe nzuri za bahari za Pangani.
Alisema endapo waandishi wa habari wataweza
kuzitumia vyema kalamu zao kwa kuutangaza mkoa huo kiutalii maisha ya
watu yataweza kubadilika ikiwa ni pamoja na biashara kuchangamka na
Serikali kuweza kupata mapato kutoka kwa wageni.
Akizungumzia matajiri kuzichangamkia fursa
zilizoko mkoani humo, Gallawa aliwataka kuwa wabunifu na kuweza kuweka
vitega uchumi na kuacha wageni kuwa waanzilishi na kuja kujutia baadae.
Alisema kuna fursa nyingi ambazo wenyeji wanaweza
kubuni na kuweza kupata vipaumbele katika sekta nzima ya uwekezaji
ikiwemo kujenga mahoteli pembezoni mwa bahari na usafirishaji wa
watalii kwa njia ya anga mbugani.
Aliwataka watu hao wenye uwezo kuwa wabunifu wa
miradi mbalimbali kwani jambo ambalo litaweza kuisaidia Serikali katika
suala zima la maendeleo na kiuchumi
Post a Comment