IVO ASEMA ANAFURAHIA MAISHA SIMBA SC…NI KAMA ALIKUWEPO KITAMBO SANA
Na Mahmoud Zubeiry, ZanzibarKIPA namba moja wa Simba SC, Ivo Mapunda amesema kwamba anafurahia maisha katika klabu hiyo na anatamani kuisaidia ishinde mataji zaidi, baada ya mwishoni mwa mwaka kuipa taji la kwanza, Nani Jembe.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Ivo alisema kwamba anafurahi namna anavyokubalika na kuheshimika kuanzia na benchi la Ufundi, wachezaji wenzake, viongozi na hata wapenzi wa Simba SC.
Anafurahia maisha Msimbazi; Ivo Mapunda amesema anajisikia kama alikuwepo miaka kadhaa Msimbazi |
“Huu ni mwanzo mzuri kwangu, najisikia vizuri na ninafurahia kuwa hapa, lakini pia hii ni changamoto kwangu kuweza kuisaidia zaidi klabu hii, ili ishinde mataji zaidi. Kwa ushirikiano wa pamoja na wachezaji wenzangu, naamini tunaweza,”alisema Ivo.
Kipa huyo wa zamani wa mahasimu, Yanga SC amesema anajisikia kama alikuwepo katika klabu hiyo miaka kadhaa iliyopita, kutokana na namna ambavyo amezoea maisha mapya haraka Msimbazi.
Amesema kwamba ana matumaini makubwa watabeba Kombe la Mapinduzi, michuano inayoendelea visiwani humo hadi Januari 13, mwaka huu.
“Tunahitaji hata sare dhidi ya KMKM ili kufuzu Robo Fainali, hilo tunaweza tena kwa kuwafunga kabisa. Tukifika Robo naamini kwa uzoefu wetu tunaweza kucheza hadi fainali. Na tukifanikiwa kufika fainali tutapigana tushinde turejee na Kombe Dar es Salaam,”alisema.
Ivo ameidakia mechi zote mbili za michuano hiyo Simba SC dhidi ya AFC Leopard ya Kenya na KCC ya Uganda ikivuna pointi nne, bila nyavu zake kuguswa hata kwa bao la kuotea. Baada ya Simba SC kuifunga Leopard 1-0 na sare ya 0-0 na KCC, itashuka tena dimbani kesho Uwanja wa Amaan, kumenyana na KMKM Saa 2:00 Usiku katika mchezo wa mwisho wa Kundi B.
Tayari Ivo amekwishaidakia Simba SC mechi tatu tangu ajiunge nayo mwezi uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya, ikiwemo ya Nani Mtani Jembe Desemba 21, mwaka jana dhidi ya mahasimu, Yanga ambayo Wekundu wa Msimbazi walishinda 3-1.
Post a Comment