MKE WA WAZIRI ATAPELIWA MIL. 280

MKE WA WAZIRI ATAPELIWA MIL. 280

Ikupa Mwakanjuki, mke wa waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Brigedia Adam Mwakanjuki, ametapeliwa shilingi milioni 280.


Waliomtapeli Ikupa ni vijana wanne ambao inadaiwa ni matapeli wazoefu jijini Dar es Salaam na kwenye baadhi ya mikoa ya Tanzania, wakitumia ‘triki’ ya uganga wa kienyeji.


Vijana hao wakijifanya waganga wa kienyeji, walimfuata Ikupa na kumwambia kwamba wangeweza kumfanya atajirike zaidi kwa njia za mizimu.

Watuhumiwa wote wanne wa utapeli huo wameshakamatwa lakini gazeti hili limepata majina ya wawili, wa kwanza akifahamika zaidi kwa jina la Silver na mwingine ni Mwang’ombe .


Chanzo chetu kilisema kuwa baada ya mwanamke huyo kupewa maneno ya ulaghai, aliingilika lakini akawa hana fedha ambazo ‘waganga’ hao walizihitaji.


“Mama aliposema hana fedha, wale matapeli walimwambia anazo mali ambazo anaweza kuuza na kupata kiasi cha fedha kinachohitajika,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:


“Mama alisema analo shamba, wakamshawishi auze. Mama naye sijui aliwekewa nini, akawa anafanya kila kitu kutokana na maelekezo ya wale matapeli.


“Kweli aliuza shamba lakini fedha zote alikabidhi kwa wale matapeli. Siku zikapita, haoni mabadiliko yoyote, ghafla akamuona Mwang’ombe anaendesha gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser Prado.


“Hapo ndiyo akashtuka, Mwang’ombe bila woga, akarudi tena kwa mama akamwambia zinahitajika fedha nyingine kwa ajili ya sadaka kwa yatima.


“Akiwa na wenzake, wakamshawishi auze shamba lingine zipatikane japo shilingi milioni 100 ili maisha yaanze kubadilika kwa kasi. Hapo ndipo akatushirikisha ndugu, tukagundua huo ni utapeli. 


Tukaamua kulifikisha hili suala kwenye vyombo vya sheria.”
Habari zaidi zinasema kuwa Ikupa kwa ushawishi wa ndugu zake, alifikisha malalamiko yake mpaka makao makuu ya jeshi la polisi na inadaiwa kuwa IGP Said Mwema aliagiza ma-RPC wote kufanya juu chini na kuwaweka nguvuni watuhumiwa.


“Hii ishu ni ya juu, sisi tumetumwa tuwakamate, tukishafanikiwa tutawakabidhi watuhumiwa kwa maofisa upelelezi makao makuu,” mmoja wa maofisa wa jeshi la polisi Kinondoni, alilinong’oneza gazeti hili.


Septemba 18, mwaka huu, saa 8 usiku, Mwang’ombe bila kujua kama yupo mtegoni, alipaki Prado lake lenye namba za usajili T940 CLX, Corner Bar, Sinza Afrika Sana, Dar es Salaam.


Alipopaki hapo, alichagua kiti ili apate ‘kuzila bata zake’ lakini eneo hilo, alikuwepo kaka mdogo wa Ikupa ambaye alitoa taarifa polisi na mara moja, gari lake likazingirwa kabla ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Kijitonyama, Mabatini.


Uwazi lilikuwepo wakati Mwang’ombe anakamatwa Corner Bar na lilipofuatilia, liligundua kwamba mtuhumiwa huyo alimtaja Silver kwamba naye ni mhusika.


Oparesheni ikitekelezwa na maofisa upelelezi makao makuu, ilifanikisha kukamatwa kwa Silver eneo la Kimara Baruti, usiku huohuo na siku iliyofuata, watuhumiwa wengine wawili walitiwa nguvuni kisha shauri likarejeshwa Oysterbay kwa utekelezaji wa mkondo wa kisheria.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camillius Wambura, alilithibitishia gazeti hili kwamba tukio hilo lipo mezani kwake.


“Tupo kwenye uchunguzi, kuna vitu tunakamilisha halafu baadaye tutafanya mawasiliano na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili kwenda mahakamani,” alisema Wambura.


Ikupa alipopigiwa simu, alipokea mtu wake wa karibu ambaye alisema: “Kama mama atataka kuzungumza na wewe atakupigia.”


Baada ya hapo hakupokea tena simu.
Utapeli kwa njia za uganga, mitandao ya simu, katika mashine za fedha (ATM) na kadhalika, umekuwa ukishika kasi nchini ingawa jeshi la polisi limekuwa likijipambanua kwamba linashughulikia kwa nguvu kubwa.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger