Lema aibwaga serikali
MBUNGE wa
Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), jana alitikisa Jiji la Arusha
baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumfutia kesi ya uchochezi
iliyokuwa ikimkabili.
Lema
alidaiwa kutoa kauli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alienda
kwenye Chuo cha Uhasibu Arusha kama anaenda kwenye sherehe za kuaga
mtoto wa kike “send off”.
Uamuzi huo
ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Devota Msofe baada ya wakili wa
serikali, Eliananyi Njiro, kutumia kifungu cha 20 kifungu kidogo cha 1
cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kuliondoa shauri hilo ambalo
lilikuwa lianze kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo. Upande wa serikali
ulipanga kuleta mashahidi tisa.
Wafuasi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliofurika mahakamani hapo
kusikiliza mwenendo wa kesi hiyo waliupokea uamuzi huo kwa shangwe
kubwa.
Akizungumza
nje ya mahakama mara baada ya uamuzi huo, Lema alisema kuwa alikuwa
anajua shauri hilo ni la kutengenezwa ndiyo maana mashahidi wengi
walikuwa ni polisi.
“Ni kama
nimeshinda kesi, na Mungu ameendelea kutupigania, na tutaendelea
kupambana kutafuta haki bila hofu maana miili yetu na nafsi zetu
zimeishapoteza maumivu kwa sababu ya mateso yaliyojaa uongo na hila.
“Tutaendelea na kelele zetu za kupigania haki bila kurudi nyuma huku uvumilivu ukiwa nguzo yetu kubwa,” alisema Lema.
Hata hivyo,
alikiri kutamka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo alienda Chuo cha
Uhasibu kama anaeenda kwenye “send-off” kwani yeye ndiye alimpigia simu
akimtaka afike kusikiliza kero za wanachuo, lakini hakulipa uzito
unaostahili suala hilo hasa ikizingatiwa kuwa pale kuna mwanachuo
alikuwa amepoteza maisha.
Lema alisema
kuwa wanaweza kuwa wamemfutia kesi hiyo ili kesho wamfungulie nyingine
jambo alilodai kuwa yuko tayari kwani anaelewa kuwa lengo ni kutaka
kumuogopesha ili aache kuwatetea wananchi kitu alichodai kuwa
hawatafanikiwa kwani tayari ana ganzi mwilini mwake, hivyo haogopi kufa,
kesi wala kufungwa.
Kwa upande
wake wakili wa Lema, Method Kimomogoro alisema kuwa ni vema kama
serikali ingeamua kutumia busara ya kuona hakuna kesi toka awali, hivyo
wasingefungua kabisa shauri hilo lililopoteza muda wa mahakama na mteja
wake, kwani hata maelezo ya kesi yalionyesha dhahiri hakukuwa na kosa la
uchochezi.
Alisema kuwa
sheria inaruhusu kumfurahia, kumkejeli au kumzomea mtu, ndiyo maana
hata bungeni wanaonekana waheshimiwa wakizomeana na kurushiana vijembe,
na akadai hata kauli iliyodaiwa kutolewa na Lema dhidi ya mkuu wa mkoa
ilikuwa kijembe tu.
Kimomogoro
alilitaka Jeshi la Polisi kutenda kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku
akiwataka warudi kwenye hoja ya msingi na wawaeleze wananchi endapo
wameshawakamata waliohusika na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu
Arusha.
Awali,
ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Aprili 24, mwaka huu, mshtakiwa Lema
akiwa eneo la Freedom Square ndani ya Chuo cha Uhasibu, alitoa maneno
ya uchochezi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
Maneno hayo
yanayodaiwa kutamkwa ni kinyume na kifungu cha 390 sura ya 35 cha sheria
ya kanuni ya adhabu, marejeo ya mwaka 2002 .
“RC anakuja
(Chuo cha Uhasibu) kama anaenda kwenye send-off, hajui chuo kilipo wala
mauaji ya mwanafunzi wa chuo hicho... (RC) Ameshindwa hata kuwapa
(wanafunzi) pole kwa kufiwa na amesema hawezi kuongea na wanafunzi wasio
na nidhamu.” Yalinukuliwa baadhi ya maneno yaliyodaiwa kuwa yalitamkwa
na Lema.
Kauli hizo
zinadaiwa zilipandisha hasira za wanafunzi ambao walianza kumrushia mawe
na chupa Mkuu wa Mkoa, Mulongo alipokuwa akiwahutubia kuhusiana na
tukio la kifo cha mwanafunzi, Henry Koga kilichotokea Aprili 23, mwaka
huu.
Post a Comment