Jeshi la Polisi wilayani Handeni lashukuru msaada wa sare za Ulinzi Shirikishi
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
MKUU wa Jeshi la Polisi
wilayani Handeni, mkoani Tanga, OCD Zuberi Chembera, amewashukuru wadau
waliojitokeza kusaidiana na jeshi lao kuhakikisha kuwa kunaanzishwa Polisi
jamii.
OCD Handeni, Zuberi Chembera, akionyesha sare za Ulinzi Shirikishi kwa baadhi ya vikundi vilivyoanzishwa wilayani humo.
Katika kuanzishwa huko,
wafanyabiashara Adolf Lyakundi na Kareem Abdulsalim, walijitolea kununua jezi
zinazotumiwa na vijana hao wa ulinzi shirikishi.
Akizungumza na Handeni Kwetu
Blog, OCD Chembera, alisema kuwa jeshi haliwezi kufanikiwa kuleta amani kama
hakuna ushirikiano wa wadau na wananchi kwa ujumla.
Alisema kwa kujitokeza wadau
hao na wengine watakaokuja mbele ya safari, kila kitu kitakuwa kizuri na
kuwafanya wananchi waishi kwa amani na utulivu wa aina yake.
“Hawa wenzetu wamejitokeza
kununua sare zinazotumiwa na polisi jamii kwa ajili ya kushirikiana nao kulinda
usalama katika mitaa mbalimbali, huku tukiamini kuwa ni mwanzo mzuri.
“Kwa pamoja wamenunua pea 25,
hivyo sisi kama jeshi la Polisi tunawashukuru wenzetu hawa na hakika kitendo
hiki kitaleta faida kubwa katika jamii yote, hususan wakazi na wananchi wa
Handeni,” alisema.
Post a Comment