WAZIRI
Mkuu, Mizengo Kayanda Peter Pinda, atakuwa mgeni rasmi katika kilele
cha maadhimisho ya sherehe za Siku ya Mara, maarufu kama (Mara Day),
zinazofanyika katika wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara kuanzia Septemba
jana hadi Septemba 15, mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John
Gabriel Tupa, alisema madhumuni ya maadhimisho hayo ni kushuhudia tukio
kuu la kuhama kwa makundi makubwa ya nyumbu kutoka Hifadhi ya Masai Mara
kwenda Serengeti.
Alisema
lengo jingine ni kuuenzi Mto Mara, ambao asili yake ni kutoka milima ya
Mau nchini Kenya na ambao hupitia katika mapori ya akiba na wanyama
walioko katika hifadhi hiyo hutegemea maji ya mto huu.
“Kwa
kutambua umuhimu wa bonde hilo, kikao kilichofanyika mwaka juzi mjini
Kigali, Rwanda kiliamua kila mwaka yafanyike maadhimisho ya Siku ya Mara
na mwaka jana wenzetu wa Kenya walifanya sherehe hizi katika sehemu
moja iitwayo Muroti na mwaka huu ni zamu yetu,’’ alisema Tupa.
Alifafanua
kuwa katika maadhimisho hayo wamealika wageni 110 na kati ya hao wageni
200 watatoka nchi jirani ya Kenya wakiwamo mawaziri wa maji, Tamisemi,
Maliasili, Mazingira - Ofisi ya Makamu wa Rais na wadau mbalimbali wa
mazingira nchini.
Mkuu
huyo alibainisha kuwa faida za maadhimisho hayo ni kuimarisha
ushirikiano, uhifadhi wa bonde la Mto Mara, kuleta mwamko kwa Watanzania
ili waweze kufahamu uhifadhi na utalii hasa wa ndani.
Alitoa
wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuhudhuria sherehe hizo ili waweze
kushuhudia namna mkoa huo ulivyojiandaa, pia watapata fursa ya
kutembelea mabanda na kujionea mambo mbalimbali.
Kwa mjibu wa Tupa, kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni: “Mara Mali Yetu, Urithi Wetu Tuutunze."
Post a Comment