Serikali ya kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga yaweka ushuru kwa wavunja mawe

Serikali ya kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga yaweka ushuru kwa wavunja mawe

VIJANA na wakazi wa kijiji cha Komsala, Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni mkoani Tanga, wanaoishi kwa kazi ya kuvunja mawe sasa watakutana na kazi nzito ya kulipishwa ushuru kutokana na kazi yao hiyo inayotumia nguvu nyingi kuifanya.
 
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu.
 
Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa kijijini hapo, serikali ya kijiji imeweka bango la kuonyesha kuwa kila tripu moja ya mchanga, kokoto na mawe makubwa italazimika kulipiwa ushuru.
Mkazi huyo alisema kuwa tangazo hilo linaanzia kwa shilingi 5000, huku likitajwa kuwa kama mzigo mwingine mzito kwa wananchi hao wa kijiji ambao wengi wao wakiwamo vijana wanaishi kwa kazi ya kuvunja mawe mlimani kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Ni tofauti na maeneo mengine ambayo wananchi wake hasa vijana wanaishi kwa kazi ya kulima vibarua, kukata mkaa na nyinginezo, Komsala wao wanaishi kwa kuvunja mawe yanayouzwa katika wilaya ya Korogwe na kwingineko.
Tayari hatua hiyo imedaiwa kuibua mkanganyiko mkubwa, ikiwa ni mwendelezo wa malumbano kati ya serikali ya kijiji na wananchi wake, hasa vijana.
Ni mapema mwaka huu idadi kubwa ya vijana iliporudisha kadi za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa madai kuwa inachoshwa na uendeshwaji mbovu wa kijiji hicho pamoja na maamuzi ya kutoka ngazi ya wilaya.
“Hatujui kitakachoendelea baada ya tangazo hili kuwekwa maana ni dhahiri halitawafurahisha vijana kwasababu fedha hizo ni nyingi na hawa wananchi wanafanya kazi ya mawe kwa kutumia nguvu zao nyingi, sasa inashangaza mtu anaweka ushuru bila hata kuwasaidia japo vifaa vya kuwafanikishia kaziz hiyo.
"Hapa watu wanaumia, wanamwaga jasho jingi, sasa inashangaza kuona fedha zao zinahitajika, wakati kuna vyanzo vingi vya mapato, kama vile migahawa, magenge, maduka na mengineyo, ikiwamo ardhi,” alisema.
Kwa bahati mbaya hatukuweza kupata sauti ya Mwenyekiti wa kijiji hicho, lakini jitihada zinafanywa ili azungumzie sakata hilo la kuweka ushuru wa mawe kwa kila tripu itakayouzwa kutoka mlimani.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger