Kichanga chafariki kwa kukanyagwa na pikipiki

Kichanga chafariki kwa kukanyagwa na pikipiki 

 

MTOTO wa miezi minne, Dora Ramadhani, mkazi wa Kijiji cha Mtumba, Tarafa ya Mlalo, wilayani Lushoto, amefariki dunia baada ya kuanguka kutoka kwenye mbeleko na kukanyagwa na pikipiki.
Mtoto huyo aliyekuwa amebebwa na mama yake, Suzani Francis (32) alidondoka baada ya mbeleko kujisokota kwenye tairi ya nyuma ya pikipiki waliyokuwa wamepanda na kuangukia barabarani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa 9:30 jioni na kwamba baada ya mtoto huyo kuanguka alikanyagwa na pikipiki hiyo na kusababisha mauti yake.
Kamanda Ndaki alisema pikipiki hiyo T 395 CCG Fecon ilikuwa ikiendeshwa na Leonard Turo (28), mkazi wa Lukozi, wilayani Lushoto.
Alisema dereva huyo anashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo unaendelea. Mwili wa kichanga hicho umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri kuwa makini wawapo barabarani, na madereva wanapaswa kuhakikisha abiria wanaowabeba wamekaa kwenye hali ya usalama kabla na wakiwa safarini.
Chanzo;Tanzania Daima
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger