MANDELA KUENZIWA KATIKA IBADA KUBWA
Dunia inaendelea kuomboleza kifo cha mzee Nelson Mandela. Jana rais wa
Afrika Kusini Jacob Zuma alitangaza siku 10 za maombolezo kwa Mandela
aliyefariki Alhamis usiku akiwa na umri wa miaka 95.
Maelfu ya watu wameweka maua kuonyesha mapenzi yao kwa Mandela
Ikulu ya Marekani imesema kuwa rais Barack Obama na mkewe Machelle
watakwenda Afrika Kusini wiki ijayo kuungana na viongozi wengine wengi
wa dunia, katika ibada ya kumuaga Nelson Mandela. Obama ambaye mwenyewe
ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani, ataambatana na watangulizi wake
wawili, George W Bush na Bill Clinton, ambao pia watasindikizwa na wake
zao.Mwili wa Mandela utawekwa katika jengo la serikali kwa muda wa siku tatu, kutoa fursa kwa wananchi wa Afrika Kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi waliyempenda. Baadaye mwili wake utasafirishwa kwenda kuzikwa mahali alipokulia Mandela, Qunu.
Ibada ya kumkumbuka Mandela
Jana maelfu ya raia wa Afrika kusini kutoka matabaka yote na rika zote walishiriki katika ibada ya pamoja ya dini mbali mbali, ambayo ilifanyika mjini Cape Town mahali ambapo Mandela alitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kuachiwa huru kutoka jela.
Mayor wa jiji la Cape Town Patricia de Lille alisema katika ibada hiyo kuwa watu wa mji huo, weusi kwa weupe, wahidi na wenye damu mchanganyiko, wanaungana kwa mshikamano kumuenzi Nelson Mandela na kukumbuka mchango wake kwa nchi yao.
Askofu mkuu wa zamani wa kanisa la Angikani nchini Afrika Kusini Desmond Tutu ambaye kama Mandela naye ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Amani, akijipangusa machozi ya huzuni alimsifu Mandela na kusema alikuwa alama ya umoja tangu alipoachiwa huru kutoka gerezani.
Kifo cha Mandela chaiunganisha dunia
Nchi kadhaa ulimwenguni zilitangaza maombolezo kwa kifo cha Nelson Mandela. Bendera zilipeperushwa nusu mlingoti katika baadhi ya nchi hizo, zikiwemo za kiafrika, Marekani, Ufaransa na Uingereza, na kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
India ilitangaza siku tano za maombolezo, na mnara maarufu wa mjini Paris, Eiffel, ulimeremeta kwa rangi za bendera ya Afrika Kusini kwa heshima ya Madiba.
Pande zenye misimamo tofauti kihistoria zimezungumza kwa sauti moja kumsifu Mandela; Wapalestina na Israel, Dalai Lama na China, Marekani na Iran wote wamemsifu kuwa mtu aliyetetea haki na usawa.
Ibada ya kumuaga Nelson Mandela ambayo itafanyika Jumanne ijayo kwenye uwanja wa mpira mjini Johannesburg inatarajiwa kuwa mojawapo ya mikusanyiko mkubwa ya watu maarufu kuwahi kutokea.
Post a Comment