KIGOMBE BINGWA WA KOMBE LA MKONGE CUP 2013
TIMU ya Shamba la Mkonge la Kigombe mkoani Tanga leo
wameibuka na ubingwa wa Kombe la Mkonge Cup mara baada ya kuibamiza China Farm ya
Morogoro mabao 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye dimba la soka
Mkwakwani.
Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani mkubwa
ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko hakuna timu iliyoweza kuona lango
la mwenzie,kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya mashambulizi kwa timu zote.
Wakionekana kujipanga na kujiimarisha vilivyo,Kigombe
waliweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa China Farm na
kufanikiwa kuandika bao lao la kwanza dakika ya 56 kupitia Said Yasin kwa njia
ya penati iliyotokana na mshambuliaji wa China Farm kumchezea faulu eneo la
hatari Abdallah Maduba.
Kutokana na hali hiyo ilimlazimu mwamuzi wa mchezo
huo,Ibrahimu Kidiwa “Mdudu”kuamuru ipigwe penati na ndipo ilipofungwa kiufundi
na mchezaji huyo ambaye pia aliweza kutengeneza nafasi nyingi kwa timu hiyo.
Baada ya bao hilo,China Farm waliweza kujipanga na kuanza
kufanya mashambulizi ya ,mara kwa mara langoni mwa Kigombe na kuweza kufanikiwa
kusawadhisha bao hilo dakika ya 70 kupitia kwa Peter Bukulu ambaye aliweza
kuunganisha krosi iliyopigwa na Rashid Paulo.
Mpaka dakika 90 zinamalizika timu hiyo zilitoka nguvu sawa
na kuongezwa dakika 30 na mwamuzi wa mchezo huo ambazo hazikuweza kuzaa matunda
yoyote ndipo ilipoamuliwa kupigwa mikwaju ya penati.
Katika hatua hiyo ya matuta ndipo timu ya Kigombe ilipoweza
kuibuka na ushindi kwa kufanikiwa kufunga penati 4-3 dhidi ya wapinzani wao
China Farm kitendo ambacho kilipelekea mashabiki wa timu hiyo kulipuka kwa
shangwe na nderemo uwanja mzima.
Akizungumzia mashindano hayo,Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano,Lai Mpuma alisema mwaka huu yalionekana kuwa na msisimuko mkubwa
iliyotokana na timu nyingi shiriki kufanya maandalizi kabambe na hivyo
kupelekea kutokutabirika kuwa nani atachukua ubingwa.
Post a Comment