MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga, imetakiwa kuweka
mazingira rafiki ya kibiashara ambayo yatawafanya wafanyabiashara
wasiukimbie mkoa huo.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa
Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Tanga, Paul Bwoki wakati akisoma
risala yake kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi
iliyofanyika jijini hapa.
Alisema wafanyabiashara wengi wanadaiwa kuikimbia bandari ya Tanga na
kutumia ya Dar es Salaam na Mombasa kutokana na huduma inayotolewa na
TRA kwenye bandari hiyo.
“Chemba ya Biashara ya Mkoa wa Tanga tunaomba TRA iwe na mazingira
rafiki ya kibiashara, sio kunyanyasana, lazima suala la kuheshimiana
lipewe kipaumbele na kufahamu kwamba sisi tuna nia moja ya kufanya
biashara na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” alisema
Bwoki.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendegu, ambaye alikuwa akimwakilisha
Mkuu wa Mkoa, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, aliitaka TRA kuboresha
huduma zake ili kuwafanya
walipakodi kundelea kulipa kwa hiari.
Dendegu alitumia nafasi hiyo kutangaza vita dhidi wanaokwepa kulipa kodi wakitumia bandari bubu na kulikosesha taifa mapato.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Nyonge Mahayu, alisema TRA ilishindwa
kufikia lengo la makusanyo yake kwa mwaka 2012/2013, lakini makusanyo
halisi kwa kulinganisha na mwaka 2011/2012 yameongezeka kwa asilimia
13.
Chanzo;Tanzania Daima
|
Post a Comment