TUNDU LISSU AMJIBU RAIS JK "HOTUBA YA RAIS IMEJAA MANENO YA KUAMBIWA"

TUNDU LISSU AMJIBU RAIS JK "HOTUBA YA RAIS IMEJAA MANENO YA KUAMBIWA"

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema hotuba ya kila mwezi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa siku tatu zilizopita, imejaa maneno mengi ya kuambiwa hasa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, ikiwa ni pamoja na uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu wa Chadema, Lissu alisema kauli zilizotolewa na Rais za kumshutumu yeye (Lissu) kuzungumza uongo bungeni, kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zilikuwa zakuambiwa, hazina ukweli wowote.

 “Pengine rais Kikwete angesoma hotuba yangu niliyoitoa bungeni asingezungumza vile kuhusu mimi.”

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa  Rais hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na  Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Rais Kikwete alisema kauli hiyo ya Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa Lissu alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.

Katika maelezo yake ya jana, Lissu alisema kuwa alipinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba kwa sababu hata wakati akiteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kupelekewa majina na taasisi mbalimbali, alifanya uteuzi wa watu ambao hawakupendekezwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo TEC na CCT.

Lissu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala alisema kamati hiyo ilipokutana na wawakilishi wa TEC na CCT (majina yanahifadhiwa kwa kuwa hatukuwapata kuthibitisha hilo), wawakilishi hao walikiri wazi kuwa majina waliyoyapendekeza sio ya watu walioteuliwa na Rais.

“Sasa hapo uongo na uzandiki wangu ni nini, labda hao wawakilishi wa TEC na CCT walisema uongo, hata wawakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania nao waliieleza kamati kuwa majina waliyoyapendekeza, sio ambayo Rais aliteua” alisema Lissu.

Alisema kuwa Rais amemshutumu bila kuujua ukweli, kusisitiza kuwa kama angesoma hotuba yake aliyoisoma katika mkutano wa 12 wa Bunge, asingezungumza maneno hayo dhidi yake.


“Ndio maana katika hotuba yake rais Kikwete alikiri wazi kwa kusema, nimeambiwa, nimesikia, nimeelezwa ukweli ni kwamba wasaidizi wake wamemdanganya,” alisema Lissu.

Source:Mwananchi
Udaku Specially Blog
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger