NA MWANDISHI WETU, HANDENI
SERIKALI Kuu kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya
Wilaya Handeni na Mkoa mzima wa Tanga, wameombwa kuingilia kati mgogoro mzito
wa ardhi katika kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, ili kuepusha hatari
inayoweza kutokea, ikiwamo vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Hayo yamesemwa juzi na wananchi wa kijiji hicho katika
mkutano ulioandaliwa na taasisi ya Handeni Kwetu Foundation inayofanya ziara
katika maeneo mbalimbali, hususan ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, baada ya
kuzinduliwa Mei 8 mwaka huu.
Wakizungumza kwa uchungu mkubwa, wananchi hao walisema kuwa
hali ni mbaya, maana kijiji chao kimeendelea kutekwa na kubaki eneo dogo
lililoanza kuibua chuki za wazi kwa wananchi.
Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Alhaj Ally Yasin Ling’ande,
alisema kiuhalisia hakuna kijiji cha Komsala, kwakuwa hawana eneo la ardhi, hasa
baada ya wilaya Korogwe kuingia kwenye eneo lao kwa kufikia hata kujenga mnada
wa ng’ombe.
“Ukiaangalia usawa palipojengwa mnada, utaamini kuwa hata
kwenye shule ya Msingi Komsala pia patakuwa ni eneo la Korogwe, ingawa si
sahihi kulinganaa na ramani ya mwaka 1978, jambo linaloonyesha kuwa huu ni
mzozo utakaoweza kumwaga damu,” alisema.
Naye William Seif alisema mbali na mipaka hiyo kuwa tata, pia
kumekuwa na idadi kubwa ya wageni kumiliki heka zaidi ya 130 na bado wanaingia
kwa wenye heka tatu wakiamini kuwa uwezo wao kifedha unawafanya wamudu kesi
zinazoendeshwa kwenye mabaraza ya Kata na wao kupata haki.
“Masikini akionewa anakimbilia kwenye Bazara la Kata, lakini
huko kumekuwa na danadana nyingi, ukizingatia kuwa siku zote mkono mtupu
haulambwi, ndio maana tunaoimba serikali ya wilaya ya Handeni, mkoa na wadau
wengine wa ardhi kuja kujionea bomu hili linalosubiriwa kuripuka hapa kwetu,”
alisema.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bashiri
Wabu, alisema kuwa ardhi katika kijiji chao imeuzwa kiholela kwa watu wenye
nazo bila kufuata sheria za ardhi, ikiwamo ya kuandaa mkutano wa wananchi wote.
“Kuna watu hawana maeneo kabisa ya kulima, wakati watu
wachache wanamiliki maeneo makubwa ambayo hata kuyalima yote hawana uwezo huo,
jambo linalokera na kuudhi mno kila tunapoliangalia suala hili katika kijiji
chetu,” alisema Wabu, akiungwa mkono pia na Hemed Ngona, Kombo Twaha, wakisisitiza
kuwa sheria za ardhi na utawala bora hazifuatwi katika kijiji chao.
Katika mkutano huo ulioanza saa 9 alasiri na kumalizika saa
12 jioni, ulihudhuriwa na watu wengi, huku idadi kubwa ikiegemea katika kero ya
ardhi na mipaka.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Komsala anayemaliza muda wake,
Mwanaidi Said, alisema kero kubwa katika kijiji hicho ni mipaka iliyoshindwa
kutatuliwa na viongozi wa juu, licha ya kupeleka malalamiko yao mara kadhaa.
“Kijiji cha Komsala sasa ni kama kitongoji tu, maana
kimechotwa katika pembe zote na ndio maana hata wenzetu wa Korogwe wamekuja
kujenga mnada wa ng’ombe kwa madai kuwa ni kwao, jambo ambalo hata mwenyekiti
atakayefuata litamuumiza kichwa,” alisema na kuwafanya wananchi wapatwe na hofu.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo aliyetumia muda huo kuaga
wananchi wake, sekeseke la mipaka limeshindwa kutatuliwa, huku akiwataka
viongozi kulipa kipaumbele kabla ya matatizo hayajakikumba kijiji chao pale
wananchi hao watakapotafuta haki yao.
Naye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, aliwashukuru
viongozi wa serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa kuwapa
ushirikiano, ikiwamo kuruhusu kutembelea katika vijiji mbalimbali kutoa elimu
ya uraia na kuhamasisha utawala bora.
“Naomba niwatoe hofu Watanzania wote kuwa mikutano hii ya
hadhara hairatibiwi na chama chochote cha siasa, hivyo tunaomba tushirikiane
kwa ajili ya kufanikisha maendeleo, hasa kama wananchi watahudhuria mikutano
wanapoitwa na viongozi wao,” alisema.
Ziara ya Handeni Kwetu Foundation ilianzia Kata ya Misima,
ambapo wananchi wengi wameiunga mkono taasisi hiyo yenye lengo la kuwakomboa
wananchi kwa kutoa elimu na kuhamasisha maendeleo ya jamii.