ASKOFU KILAINI, NZIGIRWA WAZUNGUMZIA TUHUMA
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini.
Askofu
Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini amekiri kupokea Sh80.5
milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira akisema
si mara yake kwa kwanza kupokea fedha kutoka kwa mfanyabiashara huyo
kwa kuwa mara nyingi huwa anachangia kwa uwazi miradi ya jamii.
Askofu
huyo alikuwa akizungumzia Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), iliyosomwa bungeni juzi ikimtaja kuwa ni miongoni mwa
viongozi wa dini na watu wengine waliopokea mabilioni kutoka katika
akaunti ya escrow.(P.T)
Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira.
Katika
ripoti hiyo, Zitto aliwataja viongozi wengine wa dini walioingiziwa
fedha katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki kuwa ni
Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimanye
Simon (Sh40.4 milioni).
Akizungumza
kwa simu jana, Askofu Kilaini alisema Rugemalira hupendelea kuchangia
kwa uwazi miradi ya kijamii na si yeye peke yake aliyempatia mchango,
bali kuna watu wengine wengi ambao wameshampatia na kazi yake ni
kuipokea na kuifikisha sehemu husika.
Hata hivyo, kabla hajafafanua zaidi hoja yake, simu ilikatika na baadaye hakupatikana tena.
Hata
hivyo, jana askofu huyo alinukuliwa na Gazeti la Mawio toleo la jana
akisema fedha alizozipokea kutoka kwa Rugemalira ni kwa ajili ya miradi
mbalimbali inayoendeshwa na Kanisa Katoliki.
"Ndiyo
nimepokea fedha kutoka kwa James na hii siyo mara ya kwanza, kwani mara
nyingi amekuwa akichangia miradi mbalimbali ya kijamii," alisema Askofu
Kilaini.
Alipotakiwa
na gazeti hilo kuwataja wengine waliochangia kanisa lake na kama nao
wamechanga kutoka kwenye fedha za akaunti ya escrow, alisema yeye hayumo
kwenye michango hiyo.
Alipoulizwa
anawezaje kusema hayumo kwenye orodha ya waliopewa fedha kutoka akaunti
ya escrow wakati anakiri kuwa aliingiziwa mamilioni ya shilingi na
Rugemalira, alisema michango inayoletwa kwake haina siri, hivyo wezi
halisi ndiyo wakamatwe.
"Michango inayoletwa kwangu haina siri, shikeni wezi halisi," alisema.
Askofu Nzigirwa
Kwa
upande wake, Askofu Nzigirwa ambaye alirithi kiti cha Kilaini, cha
Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam ameeleza kushtushwa kwake na
ripoti ya PAC iliyomtaja yeye na Kilaini kuhusika katika uchotwaji wa
Sh306 bilioni za escrow.
Hata
hivyo, kiongozi huyo alisema anaandaa taarifa itakayofafanua kwa kina
namna ambavyo fedha hizo zinazodaiwa zilitoka katika akaunti ya escrow
zilivyoingizwa katika akaunti yake pamoja na hoja na maswali mengi
yanayoulizwa na wananchi hasa waumini wa Katoliki kuhusiana na tuhuma
hizo.
"Hizo
taarifa zimenishtua sana. Bado nashangaa inakuwaje mimi naambiwa
nimechota fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow," alisema
Nzigirwa alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.
Nzigirwa
alisema anachofahamu hadi sasa fedha zilizoingizwa katika akaunti yake
hazihusiki na escrow lakini atafanya uchunguzi ili kupata undani wa
fedha hizo na majibu yote yatakuwa katika taarifa atakayoitoa kwa vyombo
vya habari siku yoyote kuanzia leo.
(CREDIT: MWANANCHI)
Post a Comment