Kwani
tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010
kuwa kila shule zake za msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili
kuwenza kuwaandaa wanafunzi kuingia na darasa la kwanza.
Awali
elimu hii ilikuwa ikitolewa kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi
mbalimbali na hata watu binafsi nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari.
Kwa sasa sera na miongozo ya elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila
shule ya msingi iwe na darasa la awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu.
Changamoto
kubwa iliyoibuka kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo ni namna
elimu hiyo inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule za
Serikali. Hivi karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya
shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
kuangalia hali ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Uchunguzi
ulibaini zipo shule ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa awali kila
mwaka hazina madarasa ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo inafanya
wanafunzi hao wadogo kufundishwa katika mazingira magumu na kudhohofisha
lengo zima la utoaji wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao hulazimika
kufundishiwa nje, yaani chini ya mti ama kwenye magofu (majengo ya shule
ambayo hayajakamilika) iwe madarasa au nyumba za walimu.
Teckla
Milanzi ni mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya. Anasema
kimsingi wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo wanasomea chini ya
mti kwa kuwa hawana darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema wakati wa
mvua ama jua kali mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo kwa siku
kutokana na hali ya hewa.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru
Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala
haya hivi karibuni.
Anasema anashukuru kwa sasa wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo
linaendelea na ujenzi shuleni hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada
ya ujenzi kukamilika na wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea
chini ya mti kama ilivyo ada.
Hata
hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo darasa hilo halina vitabu kwa
ajili ya kufundishia wanafunzi, bali kuna nakala moja moja kwa baadhi ya
masomo ambavyo vilitafutwa kwa jitihada za mwalimu mwenyewe. “Mfano kwa
vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja
moja tu, ambazo hutumiwa na mwalimu mwenyewe.
Anasema
darasa hilo licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa
fedha zinazoletwa shuleni kila mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa
tofauti na wanafunzi wengine,” anasema Bi. Teckla Milanzi.
Kwa
upande wake, Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi
Tunduru Mchanganyiko anasema madarasa ya elimu ya awali Wilayani
Tunduru yanakabiliwa na changamoto nyingi. Anabainisha kuwa madarasa
mengi likiwemo lake hawana vitabu wala miongozo ya namna ya ufundishaji
kabisa zaidi ya kila mwalimu anayefundisha kubuni nini afundishe kila
uchao. “…Kwanza licha ya kutokuwa na vifaa vingine hatuna chumba maalumu
cha wanafunzi hawa (darasa) kwa sasa tunatumia jengo la darasa ambalo
bado linaendelea na ujenzi na hata hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili
ya wanafunzi wa awali,” anasema mwalimu Christina Komba.
Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa
katika darasa lao.[/caption] “Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu,
hayana miongozo…huwa tunaanzima au ukipata hela yako wewe binafsi
unaenda kununua kitabu kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto.
Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa hata ukienda madukani katika
Wilaya yetu (Wilaya ya Tunduru) vitabu kama Haiba na Michezo, pamoja na
Sanaa hazipo kabisa madukani. Anasema uongozi wa juu wilayani
unalitambua hilo.
Batadhari
Mkwela ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka anasema usajili wa
wanafunzi wa awali kila mwaka huongezeka japokuwa bajeti ya kuendesha
elimu hiyo ni changamoto. “…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi
lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, vyenzo za
kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna
madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema Mkuu huyo wa
Shule ya Nanjoka. Hadija Makamla ni mwalimu wa darasa la awali Shule ya
Msingi Majengo. Mwalimu huyu ambaye amehitimu kozi ya kufundisha darasa
hilo, anasema anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa
hilo. Anabainisha kuwa darasa hilo lina jumla ya wanafunzi 48 lakini
hutumia darasa la wanafunzi wa kawaida maana hawana darasa lililojengwa
maalum kwa wanafunzi wa awali. “…Ninazo nakala chache kwa ajili ya
mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata kimoja…lakini kuna masomo mengine
sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na Haiba ya Michezo sina kabisa hata
mimi,” anasema mwalimu Makamla. “…Unajua watoto kwa kiasi kikubwa
wanajifunza kwa vitendo, picha na uhalisia, sasa huenda tunavyowapa ni
vikubwa zaidi au vidogo sana kwa sababu ya kubuni mada kwa baadhi ya
masomo. Dorothea George ni mwalimu wa darasa la awali shule ya Msingi
Nanjoka Wilayani Tunduru. Yeye anasema japokuwa hakuwahi kufanya kozi ya
ualimu wa awali kwa sasa amekabidhiwa darasa hilo kulifundisha katika
shule yake.
Anasema
darasa hilo kwa sasa lina wanafunzi 98 ambao wanasomea darasa moja
chini ya mwalimu mmoja. Anasema licha ya darasa hilo kuwa na madawati
kadhaa lakini si maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali bali ni ya
wanafunzi wa kubwa, hata hivyo bado kuna watoto wanalazimika kukaa chini
kwa kile kukosa madawati ya kutosha katika shule hiyo.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali
anasema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua
kutokana na changamoto anuai zinazowakabili. Hakuna bajeti inayoingia
kuisaidia elimu hiyo, ispokuwa mwaka huu waliletewa madawati kumi kwa
ajili ya elimu ya awali.
Kaimu
Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi
wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni.
“…Uendeshaji elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na
changamoto zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni
tatizo na wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii
kabisa.
Kwanza
hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate
chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali. Anabainisha kuwa watoto
pia wanatakiwa kupata uji wawapo shuleni lakini uchangiaji kwa wazazi
nao umekuwa tatizo kubwa. “…Wapo wanaochangia wengine wanagoma
tunasukumana hivyo hivyo na mambo yanasonga mbele…lakini kutokana na
uchangiaji duni kuna baadhi ya siku wanapata uji na sikunyingine
hawanywi kutokana na ugumu wa michango,” anasema mwalimu George.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko, Adam Hausi katika
mazungumzo na mwandishi wa makala haya anasema uendeshaji wa elimu ya
awali katika shule hiyo ni juhudi binafsi za mwalimu wa darasa hilo.
Anasema darasa hilo halina bajeti yoyote kutoka serikalini hivyo hakuna
vitabu na vitendea kazi vingine vinavyohitajika. “…Vitendea kazi ndio
tatizo kabisa, ila mwalimu anafundisha kwa jitihada zake na darasa
linaendelea. Alafu lina idadi kubwa sana ya wanafunzi (84) na
anafundisha peke yake…,” anasema Hausi.
Anasema
uboreshaji elimu ya msingi ni suala la ushirikiano kati ya Serikali na
jamii yenyewe lakini wakati mwingine Serikali inakwamisha juhudi hizo
kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo baadhi ya maeneo. “…Mfano sisi
tulijenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi hadi yamekamilika
ilipofika suala kuezekwa tokaomba msaada wa Serikali pamoja na
kumaliziwa ili yaanze kutumika ilikuwa kazi kweli tulizunguzwa sana hadi
tukaanza kuyatumia hivyo hivyo,” alisema.
Bi.
Thabita Farara ni Mkazi wa Kata ya Mringoti Mashariki anasema bado
mwamko wa elimu ya awali kwa wazazi ni mdogo, maana wazazi wengi
wamekuwa wakijiandaa na darasa la kwanza tu kumuandikisha mtoto. Kwa
upande wake Asha Komba Mkazi wa Tunduru Stendi anasema yeye anaitambua
elimu ya awali na kuikubali lakini ni ile inayotolewa na shule binafsi
kama za taasisi.
Lakini
ile inayotolewa kwenye shule za Serikali ni tatizo kubwa maana
hazizingatii ubora wa elimu zaidi ya kuwalundika watoto tu darasani.
“…Mimi naitambua elimu ya awali na watoto wangu wote wamepitia lakini
huwa tunawapeleka kwenye chekechea za taasisi mbalimbali kama
zinazomilikiwa na makanisa majeshi na zinginezo maana huku ndiyo kidogo
mtoto anaandaliwa…kule Serikalini kwanza unakuta darasani wapo kibao
alafu muda wote wanacheza tu si kujifunza,” anasema Bi. Komba.
Abdul Kazembe ni Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, anasema kwa sasa
kila shule ya msingi sera inaelekeza lazima iwe na darasa la awali.
Anasema hata katika usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa sasa
watoto wa mwanzo kusajiliwa ni wale waliopata elimu ya awali katika
shule husika. “…Kwa hiyo kuna umuhimu wa kila shule kuwa na darasa la
awali…changamoto sasa inakuja kwenye vitendea kazi, kwa mwaka 2013 na
kurudi nyuma uwepo wa ‘capitation’ ulikuwa pia unaelekeza watoto wa
awali wapo mule na hata tunapotoa takwimu za awali tulianza na
‘pre-primary’ (wanafunzi wa awali) hivyo wenyewe wapo, tatizo hapa ni
ujaji wa pesa yenyewe ya ‘capitation’ haitimii kama inavyo elekeza,
yaani ile wastani ya kwamba kila mtoto apate shilingi 10,000 kwa mwaka
hautimii,” anasema.
Anatolea
mfano mwaka 2013/14 kiwango cha fedha ambacho kilitakiwa kuja katika
halmashauri ya wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 366.7. Kiwango hiki ni
kile kilichoidhinishwa katika bajeti tu lakini ukirudi kwenye mahitaji
halisi ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa. Anasema kilichokuja ni zaidi
ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu ya kiasi kilichopitishwa
kwenye bajeti. Anabainisha hilo ndilo tatizo kubwa kwani hata fedha
ambazo zimepitishwa haziji kama ilivyopitishwa kwenye bajeti.
“…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika
matumizi maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni
pungufu zaidi tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate
shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,” anasema.
Anasema
kwa upande mwingine miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa. Kwa
mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni
1,715 lakini ukiangalia vyumba vya madarasa vilivyopo ni kama 900 na
kitu na mengine ni ya muda mrefu sana kiasi ambacho yanaelekea kuchakaa
jambo ambalo pia yanapungua. Aidha anaeleza kuwa ukienda kwenye bajeti
ya ujenzi wa madarasa mapya milioni 171 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa
na miundombinu mbalimbali kiasi hiki cha fedha waweza kuta kinauwezo wa
kujenga madarasa kama nane tu.
Kiasi
hicho cha fedha ni pamoja na ujenzi wa nyumba tano za walimu. Na kiasi
hicho cha fedha za ujenzi ni pamoja na kumalizia miradi viporo za nyumba
za walimu na vyumba vya madarasa. Anasema upungufu wa vyumba vya
madarasa eneo hilo ni karibia madarasa 800. “Sasa kwa ujumla unaweza
kuona kuwa miundombinu pale shuleni haitoshelezi, ni jambo la kawaida
kuona walimu wakiacha ofisi itumike kama darasa au darasa litumike kama
ofisi.
Huku
kwa awali ni changamoto zaidi maana licha ya upungufu wa vyumba hata
wazazi hasa vijijini wanashindwa kuchangia chakula (uji) kwa watoto wao
unaweza kukuta wameandikishwa wengi Januari lakini kila muda unavyozidi
kwenda watoto wanapungua na unaweza kukuta hadi mwezi Juni darasa
linapotea kabisa kwa utoro,” anasema. Kazembe anabainisha kuwa kuna
jumla ya shule za msingi 144 katika wilaya hiyo, huku shule zilizo na
vyumba maalumu vya madarasa ya awali zikiwa 16 tu.
Anasema
shule nyingine zote hazina vyumba vya madarasa ya awali na matokeo yake
ama wanatumia madarasa ya msingi kwa kupishana. Anaongeza kuwa
uhamasishaji wa ujenzi wa madarasa ya awali na umuhimu wa elimu hiyo
unatolewa kwa walimu, wazazi na kamati za shule kupitia vikao mbalimbali
ambapo mara nyingi uongozi uhimiza wazazi kuchangia zaidi nguvu zao
katika kukamilisha ujenzi wa madarasa ya awali, utengenezaji wa madawati
na upatikanaji wa chakula cha mchana na uji shuleni. “…lakini
tunaangalia sana chakula maana watoto hata kwenye mti wanaweza kukaa
wakasoma endapo wanamadawati pale au wamekaa chini kwenye kivuli,
japokuwa si mazingira mazuri sana shuleni…lakini wakiwa na chakula hata
utoro unapungua,” anasema. Anasema kwa mwaka 2013 serikali ilikumbuka
kuleta fedha kwa ajili ya ununuzi madawati ya wanafunzi wa awali, fedha
ambazo tulizigawa na kununua baadhi ya vitabu vya awali na madawati
kwenye shule ambazo zinamadarasa hai ya awali.
Shule
zilizonufaika na mgao huo ni shule za mjini Tunduru tu ambazo nyingi
ndizo zenye madarasa hai ya awali. Anasema ili kukabiliana na hali ya
upungufu wa walimu wa awali; imepitishwa walimu wa gredi ‘A’ kufundisha
madarasa hayo kwa kuwa wao mafunzo yao katika kozi hujumuisha
ufundishaji darasa la awali, tangu walioitimu mwaka 2013.
“…sasa
wakati mwingine unaweza kukuta mwalimu ni gradi A na kimsingi yeye anao
uwezo wa kufundisha darasa la awali, lakini wengine hawakubali hadi
aone ana cheti kabisa maalumu cha kufundisha darasa la awali…ukimuuliza
huyu atakwambia yeye hana taaluma ya kufundisha awali jambo ambalo si
sawa,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Msingi. “..Kwa suala la vitabu kweli
hii ni changamoto, hapo nyuma tulikuwa tunanunua vitabu wenyewe wakini
kwa sasa TAMISEMI wenyewe moja kwa moja wananunua na kuvileta.
Sasa
huku kwetu ni nadra sana kuona wazabuni wetu wanaleta vitabu vya awali
kwa sababu soko lake ni dogo sana kutokana na idadi ndogo ya uwepo wa
elimu hii ya awali eneo husika,” anasema. Hata hivyo umeona unafuu
maeneo ya mjini mzazi anatambua umuhimu wa elimu hivyo anaweza kuchonga
dawati kwa ajili ya mtoto wake lakini kwa vijijini hali ni mbaya zaidi.
Mzazi ukimwambia achangie dawati anakushangaa na pia haoni umuhimu huo.
“…Nikwambie unajua Wilaya ya Tunduru mzazi mtoto wake akifeli anafurahi
sana…tena baadhi wanaona kama ni sherehe, kwanza wakifanya mtihani tu
wa la saba barabarani akina mama wanashangilia wanaona wametua mzigo,
unaweza kujiuliza wazazi wanaoshangilia inamaana walikuwa wakiona ni
adhabu watoto wao kuwa shule?
Lakini
pia mtoto akisha faulu kwenda shule hapelekwi hadi DC aunde kamati,
atembee na hakimu na polisi kukamata wazazi wanaogoma kusomesha watoto
watishiwe ndo wanakubali kusomesha…lakini kitendo cha wazazi kukamatwa
kushikiliwa kwa kushindwa kuwapeleka watoto shule wamegeuka na
kuwarubuni watoto wao wasifaulu,” anasema. Anabainisha kuwa ni kweli
Serikali ina jukumu la elimu, lakini mzazi kwa upande wake anajukumu
zaidi, kuangalia mtoto wake anapata elimu gani na ya kiwango gani na
kama mzazi hayupo tayari basi haiwezekani na wakati mwingine inakuwa
ngumu. Kimsingi jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya
kufundishia na kujifunzia watoto wa awali zipo, lakini upatikanaji wa
fedha ndio. Salum Mtutula ni Mbunge wa Tunduru Kusini kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mbunge huyu katika mahojiano anakiri kuwa elimu ya
awali ni muhimu na msingi mzuri wa mtoto kielimu.
Anasema
mtoto anapopata elimu nzuri ya awali huwa na msingi mzuri kielimu
katika masomo yake ya mbele. “…Ili mtoto apate elimu bora ni lazima
apate elimu ya awali inayostahiki…hakiwa na msingi mbaya wa elimu ya
awali kuna uwezekano mkubwa way eye kufanya vibaya pia,” anasema
Mtutula. Hata hivyo anaishauri Serikali kuingiza suala hili katika
sheria na kanuni zake kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa ianze na
darasa la awali kwanza ndipo madarasa mengine yafuate.
“…Mimi
nitafurahi kama suala hili tutaliweka kwenye sheria au kanuni zetu kuwa
kila shule ya msingi inapoanzishwa basi lazima ianze na darasa la awali
ndipo madarasa mengine yafuate iwe shule za Serikali au binafsi,”
anasema Mbunge Mtutula.
*Imeandaliwa na: www.thehabari.com