Nimenusurika kupigwa na Wazanzibari mara mbili bungeni
Mbunge Ali Keissy akitolewa nje ya Ukumbi wa Bunge na walinzi.
Mbunge wa
Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa, Ally Keissy amesema kuwa katika uhai wake
akiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la
Katiba hawezi kusahau alivyonusurika kupata kipigo kutoka kwa wabunge wa
Zanzibar.
Alizungumza
hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyotaka kujua historia
ya maisha yake kabla na baada ya kuwa mbunge, hali ya kisiasa na
Mchakato wa Katiba ulivyokuwa.Keissy alisema kuwa alinusurika mara mbili
kupigwa na wabunge hao, huku wakimtolea lugha za kejeli na matusi.
"Kitu
ambacho siwezi kukisahau nikiwa bungeni tangu mwaka 2010 mpaka sasa ni
matukio mawili ya kutaka kupigwa. Moja ni katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano na jingine katika Bunge Maalumu la Katiba; ...haya siwezi
kuyasahau kamwe," alisema mbunge huyo.
Keissy
aliongeza: "Unajua unapokuwa bungeni, hakuna haja ya kuonyesha ubabe,
unashindana kwa hoja na unajibiwa kwa hoja. Kama mimi nimetoa hoja, basi
nanyi mjenge hoja kwa kunijibu, lakini kukimbilia kutaka kunipiga siyo
suluhisho."
Anakumbuka
matukio hayo akieleza kuwa mosi ni lile lilitokea Mei 26 mwaka huu
ambapo alinusurika kupigwa baada ya kutoa maneno yaliyodaiwa kuwa ya
kashfa kwa wabunge wa Zanzibar wakati wa akichangia Hotuba ya Bajeti ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
"Tukio la
pili lililotokea mwezi uliopita (Septemba), wakati wa vikao vya Bunge
Maalumu la Katiba, nilinusurika kipigo baada ya kupinga Rais wa Zanzibar
kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano,"alisema Keissy.
Akichangia
mjadala wa Katiba, mbunge huyo asiyeisha vituko alisema kuwa
haiwezekani Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kwa kuwa
hakuchaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara jambo lililozua tafrani
bungeni.
Hata
hivyo, Keissy alisema kuwa pamoja na matukio hayo na vitisho vingine,
hatasita, wala kuogopa kusema analoamini kuwa ni kweli.
"Kamwe
sitaogopa, nitaendelea kusema ukweli, nitaendelea kujenga hoja kwa kile
ninachokifahamu na watu wanaotaka kunipinga wawe wakipinga kwa hoja,
hapo nitakuwa tayari kuwasikiliza,"alisema.
Historia ya maisha yake
Keissy alizaliwa wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa 15-Oktoba-1954. Alihitimu darasa la nane, Sumbawanga Middle School mwaka 1965.
Baada ya
kumaliza darasa la nane, alianza kufanya shughuli mbalimbali hasa
biashara za magari ya kubeba mizigo, mabasi ya abiria na maduka ya kuuza
bidhaa mbalimbali.
Post a Comment