SIMBA SC YALAMBA SH MILIONI 60 AZAM FC MAUZO YA KAPOMBE, SHOMARY SASA MCHEZAJI HALALI CHAMAZI
Shomary Kapombe sasa ni mchezaji halali wa Azam FC |
Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imepokea Sh. Milioni 60 kutoka kwa Azam FC na imemuidhinisha kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba suala la Kapombe limemalizika na sasa kwa baraka zote huyo ni mchezaji halali wa Azam FC.
“Tumekwishamalizana na Azam FC, Kapombe sasa ni mali yao,”amesema Kaburu na kuongeza; “Na sisi pia tumetekeleza wajibu wetu kwa kuwapa mgawo wao Morogoro Youth Football Academy, (Sh. Milioni 9),”.
Wakati Simba SC inamsajili Kapombe kutoka kituo hicho cha soka Morogoro miaka mitatu iliyopita, walifikia makubaliano akiuzwa na Wekundu hao wa Msimbazi wapate asilimia 15 ya mauzo.
Azam FC ilimnunua Kapombe kwa Euro 43,000 kutoka AS Cannes na mbali na kuwalipa Simba Milioni 60 kama asilimia 40 ya fedha walizotoa kwa klabu ya Ufaransa kumnunua nyota huyo, pia wanatakiwa kumlipa wakala Dennis Kadito asilimia 20.
Kadito ndiye aliyempeleka Ufaransa Kapombe baada ya Simba SC kukubali kumtoa bure, kwa matarajio akiuzwa Ulaya itapata mgawo mzuri.
Kaburu amekabidhi hundi ya Sh. Milioni 9 kwa Morogoro Youth Football Academy kama sehemu ya mgawo wao wa mauzo ya Kapombe Azam FC |
Kapombe alikwenda Ufaransa katikati ya mwaka jana kujiunga na klabu hiyo ya Daraja la Nne, lakini Novemba mwaka huo aliporejea kuichezea Tanzania katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Zimbabwe hakutaka tena kurudi Ulaya.
Machi mwaka huu, akaanza kufanya mazoezi na Azam FC kabla ya mwezi uliopita kusaini Mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu nchini.
Post a Comment