NA BONIFACE WAMBURA,MAPUTO.
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
amesema anakiamini kikosi chake ambacho kesho (Agosti 3 mwaka huu) kinacheza
mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji
(Mambas).
Mechi hiyo ndiyo itakayoamua ni
timu ipi kati ya Tanzania na Msumbiji itakayoingia hatua ya makundi ya michuano
ya Afrika kwa ajili ya kutafuta tiketi za Fainali itakayofanyika mwakani nchini
Morocco.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa
jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao
2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde,
Niger na Zambia.
Akizungumza hapa Maputo, Nooij
amesema anaamini kikosi chake kitacheza vizuri zaidi kuliko kilivyofanya jijini
Dar es Salaam kwa vile hakitakuwa katika shinikizo la washabiki ambalo mara
nyingi hufanya wachezaji wasijiamini.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager imefikia katika hoteli ya Pestana Rovuma ikitokea
Johannesburg, Afrika Kusini ambapo ilifanya maandalizi yake mwisho, na itafanya
mazoezi leo (Agosti 2 mwaka huu) saa 9 alasiri Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao
ndiyo utakaotumika kwa mechi ya kesho.
Kikosi hicho cha timu ya Taifa leo
imeandaliwa chakula cha jioni na Balozi wa Tanzania hapa Msumbiji, Shamim
Nyanduga.
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu nao wameungana na timu leo asubuhi hapa Maputo wakitokea Lubumbashi
katika klabu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mechi itakayochezeshwa na waamuzi
kutoka Uganda wakiongozwa na Dennis Batte itaanza saa 9 alasiri kwa saa za hapa
ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 10 jioni.
Wachezaji waliopo katika kiosi cha
Taifa Stars hapa Maputo ni Aggrey Morris, Aishi Manula, Amri Kiemba, Deogratias
Munishi, Erasto Nyoni, Haruna Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Kelvin Yondani, Khamis
Mcha, Mbwana Samata, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Oscar Joshua,
Ramadhan Singano, Said Moradi, Shabani Nditi, Shomari Kapombe, Simon Msuva na Thomas
Ulimwengu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
MAPUTO
Posted by
Unknown
7:21 AM