Ummy: Nitavalia njuga bei ya gesi
NAIBU
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Ummy Mwalimu, ameahidi
kulivalia njuga suala la bei za nishati ya gesi kwa lengo la kuhakikisha
kila mwanamke wa Kitanzania ananufaika na nishati hiyo.
Naibu Waziri huyo alisema hayo alipokuwa akifungua warsha ya mafunzo
kwa madiwani wanawake kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Tanga
yalioandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tawode.
Alisema kina mama wengi wamekuwa wakitumia mkaa katika matumizi yao
ya nyumbani kutokana na kushindwa kumudu gharama za nishati ya gesi
ambayo kwa hivi sasa bei yake iko juu.
“Kwa kweli nitalivalia njuga suala hili sitakubali kumuona mwanamke
wa Kitanzania akitaabika kutumia mkaa na ikiwa tuna majiko ya gesi
tushushe gharama za majiko haya, ili kuwe na urahisi wa matumizi ya
nyumbani,” alisema Ummy.
Mkurugenzi wa Tawode, Fatuma Hamza, alisema mafunzo hayo yana lengo
la kuwafundisha viongozi wanawake kujua mbinu za utawala bora kwa
maendeleo ya wanawake na taifa kwa ujumla.
Alisema kutokana na msingi huo, taasisi hiyo imeweka kipaumbele cha
juu suala la utawala bora na usawa wa jinsia, ili kufanikisha mageuzi ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa progamu mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, aliwataka madiwani hao
wanawake kuhakikisha wanakuwa na mshikamano kwa upande wa kuwatetea
wanawake katika bajeti zinazopangwa na halmashauri zao.
Chanzo;tanzania daima
Post a Comment