Pitia tamko la Chadema dhidi ya kutekwa kwa mwenyekiti wao Temeke

Pitia tamko la Chadema dhidi ya kutekwa kwa mwenyekiti wao Temeke

 

 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko taarifa za tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Josephat Yona Patrick.

 Chama kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano
na Uhusiano, mbali ya kukemea kwa nguvu zote tukio hilo la kihuni na mengine ya
namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu, katika hatua ya sasa
kinapenda kusema yafuatayo juu ya tukio hilo ovu ;
1.   Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi juu ya tukio hilo la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke ili ukweli ujulikane na haki itendeke, kwa sheria kuchukua mkondo wake.

2.   Chama kinawataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale ambapo watu wenye hila na malengo yao, wanaanza kukihusisha chama na tukio hilo. Watambue kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa kiongozi wa chama, bado anayo maisha yake na uhusiano na watu wengine katika jamii.

3.   Jeshi la Polisi linapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na unaostahili matukio ya namna hii ambayo yanaanza kuota mizizi kutokana na watu waovu wanayoyatekeleza kutochukuliwa hatua za kisheria ambazo zingesaidia kuzuia yasitokee tena.

4.     Watanzania bado wanakumbuka kwamba hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa taarifa za kina na kuchukua hatua za kisheria ambazo zingesaidia ukweli kujulikana na haki kutendeka katika matukio ya kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Dk. Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda. Hivyo ingesaidia kuzuia
matukio mengine kutokea.

5.   Ni kutokana na jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matukio mengine ya namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa kinachoendelea ndani ya CHADEMA kwa chama kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama wasio waadilifu, kufanya matukio ya namna hiyo ili kujenga taswira ya kukihusisha chama na uhuni huo unaobeba kila sifa ya kuitwa ukatili dhidi ya binadamu.

6. Aidha kushindwa kwa Jeshi la Polisi kuwajibika ipasavyo katika kufanya uchunguzi wa matukio hayo (yaliyotolewa kama mfano hapo juu) na mengine ya namna hiyo, jeshi hilo linazidi kujiweka katika wakati mgumu wakukwepa tuhuma za baadhi ya watendaji wake kujua na kushiriki masuala haya, hususan kwa kurejea tukio la kutekwa kwa Dkt. Ulimboka.

Imetolewa jana Jumanne, Januari 7, 2014 na;

Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger