M23 yachakazwa, viongozi watimka

M23 yachakazwa, viongozi watimka

mejakomba_edffb.jpg

Kuna ripoti kwamba Kundi la Waasi la M23 ambalo limekuwa likisababisha mapigano katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), limesambaratishwa katika operesheni kali iliyoendeshwa kwa ushirikiano baina ya vikosi vya nchi hiyo na vile vya Umoja wa Mataifa.

Taarifa za kusambaratishwa kwa kundi hilo zimekuja siku chache baada ya kuzuka mapigano makali yaliyosababisha kuuawa kwa askari mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Rajab Ahmed Mlima aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa katika operesheni ya kuwaokoa raia, waliokuwa wamenasa kwenye eneo la mapigano.

Wanajeshi wa Tanzania ni sehemu ya vikosi vya Umoja wa Mataifa vya Kulinda Amani huko Congo (Monusco) vyenye askari pia kutoka Afrika Kusini na Malawi, vikiwa na kazi ya kupambana na kupokonya silaha za vikundi vya waasi wanaopigana kwenye nchi hiyo.

Mkuu wa Vikosi vya Monusco, Martin Kobler alithibitisha taarifa za kusambaratika kwa kundi hilo la M23 na kuongeza kuwa vikosi vya Serikali na vile vya UN vilikuwa vikiendesha doria katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti jana kuwa Kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa amekimbia mashambulizi kwa kuvuka mpaka na kuingia Uganda wakati majeshi ya Congo yalipokuwa yanakaribia ngome yao.
Katika taarifa yake aliyoitoa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juzi, Kobler alisema Kundi la M23 limepoteza mwelekeo.

"Ninachoweza kusema sasa tumefanikiwa kuwasambaratisha waasi na sasa vikosi vyetu kwa kushirikiana na vile vya DRC Congo vinadhibiti maeneo yote," alisema Kobler.

Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Meja Eric Komba alisema asingeweza kutoa maelezo ya kina kuhusiana na taarifa za kusambaratishwa kwa kundi hilo la waasi, kwa vile wazungumzaji wakuu wa suala hilo ni Umoja wa Mataifa.

"Kama mnavyojua sisi tumekwenda DRC Congo kwa ridhaa ya Umoja wa Mataifa, hivyo kufanikiwa ama kushindwa kwa operesheni yoyote iko chini ya Umoja wa Mataifa wenyewe. Tanzania haiwezi kusema kwamba vikosi vyetu vimewasambaratisha waasi wakati mwenye jukumu la mwisho kutoa tamko hilo ni UN wenyewe," alisema Meja Komba.
Wakati hali ikiripotiwa kuwa hivyo, taarifa zinasema kuwa kundi hilo la M23 limemeguka mara mbili na kuzaliwa kundi jingine linalojiita M18. Maofisa wa Serikali ya Uganda wamesema kuwa kujitokeza kwa kundi hilo jipya kunaashiria kifo cha Kundi la M23 ambalo kwa miaka mingi limekuwa likidhibiti maeneo yanayotajwa kuwa na utajiri wa madini.

Kundi hilo la waasi ambalo limekuwa likidaiwa kupata msaada wa kijeshi kutoka kwa mataifa ya Rwanda na Uganda, limeelezwa kuelemewa nguvu na limesalimu amri katika maeneo liliyokuwa likishikilia.

Vikosi hivyo vya M23 vilianzisha upya mapigano hayo na kufanikiwa kuteka baadhi ya miji muhimu baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani yaliyokuwa yakiendelea Kampala, Uganda.
Waasi wakimbilia porini

Baada ya kutorokwa na viongozi wao, kuna taarifa askari wa kawaida wa Kundi la M23 wamejificha kwenye misitu ya mpaka wa DRC Congo na nchi za Rwanda na Uganda.

Msemaji la Jeshi la DRC, Olivier Hamuli aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) katika eneo la mapigano karibu na Goma kuwa Kundi la M23 limedhoofika baada ya kukimbiwa na askari wapatao 40, ambao wamejificha kwenye milima ya karibu na mpaka wa Rwanda.

"Kuna kundi dogo la M23 linapigana karibu na milima ya Rwanda," alisema. "Nadhani Rwanda watapaswa kufanya uungwana na kuwakamata."

Kundi la M23 lilianzisha vita mwaka 2012 baada ya baadhi ya askari wa Jeshi la DRC Congo kuasi baada ya kutoridhishwa na utekelezaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2009, uliosainiwa na waasi hao wanaoaminika kusaidiwa na Rwanda.
DRC waandaa dua

Habari zaidi kutoka DRC Congo zinasema kuwa wafuasi wa dini ya Kiislamu katika mji wa Goma walifanya swala maalumu kwa ajili ya kuwaombea askari wa nchi hiyo na wale wa Umoja wa Mataifa waliofariki dunia kwenye operesheni hiyo.
Pia waliahidi kuandaa maandamano makubwa kwa ajili ya kushinikiza kuondoka kwa raia kutoka India na wale kutoka nchi za Ulaya kwani wanaamini ndio wamekuwa wakiwasaidia waasi kifedha.

Chanzo:Mwananchi
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger