N/WAZIRI MAKAMBA AVIPA CHANGAMOTO VIWANDA VYA CHAI BUMBULI.

N/WAZIRI MAKAMBA AVIPA CHANGAMOTO VIWANDA VYA CHAI BUMBULI.

Na Raisa Said, Bumbuli.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amevipa changamoto  viwanda vya chai vya Hekulu na Dindira kuongeza uzalishaji ili kuweza kuchukua majani ya chai kutoka kwa wakulima wa zao la chai wa Bumbuli ambao walikuwa wakihudumiwa na Kiwanda cha Mponde.

Hatua hiyo inatokana na kiwanda cha chai cha Mponde kufungwa kutokana na mgogoro baina yawakulima wa chai na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (UTEGA) na mwekezaji.

Makamba, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Bumbuli aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wakulima katika kijiji cha Tamota, kilichopo kata ya Tamota jimboni hapo, alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kiwanda cha Mponde kilivyofungwa na viwanda hivyo viwili vikiongeza uzalishaji wakulima watapata mahali pa kuuzia majani ya chai na kujipatia kipato.

Alisema kuwa hivi sasa majani ya chai ni mengi hivyo hatua ya viwanda hivyo kuongeza uzalishaji ni nafuu kwa wakulima ikiwemo kuchangia kasi ya maendeleo kwa wananchi wa maeneo hayo.

Makamba alisema kuwa alikwisha kuzungumza na menejimenti za viwanda hivyo ili viongeze uzalishaji na vifaa vya kusafirishia chai kutoka mashambani hadi kwenye viwanda.

Alisema kuwa atavishauri viwanda hivyo kuweka utaratibu wa kuchukua majani ya chai mara tatu kila wiki kwa wakulima hao ili kukabiliana ongezeko hilo la majaniya chai.

Aliwataka wakulima kuwa wavumilivu wakati huu ambapo kuna mpango wa kuweka menejimenti ya muda kama ilivyokubaliwa na serikali ili kiwanda hicho kianze kazi ya kusindika majani ya chai.

Aliwataka viongozi wa UTEGA kuacha kuwatisha wakulima kwa kuwaambia kuwa watawakomesha kipindi hiki cha majani mengi ya chai na kwamba watahakikisha wanawapigia magoti ili kiwanda kifunguliwe.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger