ZANZIBAR HAPAKALIKI...VIONGOZI WA DINI WAHOFIA ROHO ZAO

ZANZIBAR HAPAKALIKI...VIONGOZI WA DINI WAHOFIA ROHO ZAO

Na Imelda Mtema
HAKUNA lugha nyingine zaidi ya kusema Zenji (Zanzibar) sasa hapakaliki hasa kwa viongozi wa dini, achilia mbali raia wa kigeni kufuatia kushamiri kwa vitendo vya kuwadhuru kwa tindikali au silaha, Ijumaa Wikienda lina mfululizo wa mikasa na ifuatayo ndiyo ripoti kamili.
Padri Joseph Onesmo Mwang’amba akiwa hospitalini baada ya kumwagiwa tindikali.
Ukiachilia mbali mnyororo wa matukio hayo yaliyosababisha  makovu, ulemavu na vifo, tukio ambalo halijapoa ni la Ijumaa iliyopita ambapo Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui, Zanzibar, Joseph Onesmo Mwang’amba (60) kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lenye kuunga na mengine nyuma, lilijiri nje ya duka la huduma ya mawasiliano ya intaneti la Shine Shine lililopo Mtaa wa Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar ambako padri huyo alikwenda kuperuzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Afande Haji Hana alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo lilimfikisha mtumishi huyo wa kiroho kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja ambako anaendelea na matibabu.
Shehe Fadhil Suleiman Soraga baada ya kumwagiwa tindikali.
Tindikali hiyo ilimjeruhi padri sehemu za usoni, kifuani na mkono wa kulia.
Novemba 6, 2012; Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana. Alijeruhiwa usoni na mwilini.
Desemba 26, 2012; watu wasiojulikana wamlipiga risasi Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael, Mpendae mjini Unguja na kumjeruhi vibaya.
Padri Ambros Mkenda akiwa hospitali baada ya kupigwa risasi.
Faza Mkenda alipigwa risasi nje ya nyumba yake. Alikimbizwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Unguja na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar.
Februari 2013; Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa akiwa kwenye gari akielekea kanisani kuongoza ibada.
Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi aliyeuawa kwa kupigwa risasi.
Mei 23, 2013; Sheha wa Tumondo, Mohamed Omar Said alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana. Alipata majereha sehemu ya kifuani na jicho la kulia na kukimbizwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja ambapo alipatiwa matibabu ya dharura.
Agosti 8, 2013; wasichana wawili raia wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) walimwagiwa tindikali wakiwa katika matembezi ya kawaida Mtaa wa Shangani mjini Zanzibar na kujeruhiwa sehemu za uso na kifuani.
Kate Gee na Kristie Trup waliomwagiwa tindikali wakiwa katika matembezi ya kawaida Mtaa wa Shangani mjini Zanzibar.
Kufuatia mtiririko huo, habari zinadai kuwa hali ya maisha ya Zanzibar kwa sasa si shwari kwani viongozi wa kiimani wamekuwa wakitafakari upya jinsi ya kuishi visiwani humo au kurudi Bara.
Yapo madai kwamba, baadhi ya viongozi hao wa dini na raia wameingiwa hofu na wamepanga kuandamana ili kupinga hali ya hatari inayotokana na vitendo hivyo huku kundi moja lenye imani kali likitajwa kuhusika. Polisi bado inachunguza matukio yote hayo.
Source:Global Publishers
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger