LOWASSA ATOBOA SIRI..BARAZA LA MAWAZIRI LILIMPINGA
WAZIRI Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema Baraza la Mawaziri, lilimpinga asisafirishe maji kutoka Ziwa Victoria hadi wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Amesema kwamba, siku aliyowasilisha wazo hilo katika baraza hilo, mawaziri wote walimpinga, isipokuwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Mohamed Seif Khatib.Lowassa alitoboa siri hiyo jana, alipokuwa akizungumza katika harambee ya uchangiaji wa Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT, Kahama, Shiyanga.
Pamoja na hayo, alisema anayetakiwa kupongezwa katika mradi huo ni pamoja na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa kuwa alishiriki kuufanikisha.
“Niwapeni siri moja, nilipendekeza waraka wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa Rais Mkapa, naye akaniuliza, wale wakubwa tutawaweza? Nikamwambia tutawaweza, akauleta katika Baraza la Mawaziri.
“Kule mawaziri wote waliupinga, kasoro Rais Kikwete, ambaye wakati ule alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na rafiki yangu, Mohamed Seif Khatibu.
“Mzee Mkapa baada ya kusikiliza mawazo yote, akaamua fedha zitolewe, na sasa mnafaidi maji safi kutoka Ziwa Victoria,” alisema Lowassa.
Ufafanuzi huo aliutoa baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kumsifu Lowassa kwa kuleta maji mkoani humo, ambapo alisema wananchi wa Shinyanga wanayaita maji hayo kwa jina la Malowassa, yaani maji ya Lowassa.
Pamoja na hayo, wakati msafara wa Lowassa unaingia wilayani Kahama, wananchi walijaa barabarani na kumshangilia, huku baadhi wakionyesha maji kama ishara ya kutambua mchango wake katika maji hayo.
Lowassa, ambaye wakati maji yanapelekwa Shinyanga alikuwa Waziri wa Maji na Mifugo, alisema wakati alipokuwa katika juhudi za kupinga mkataba wa zamani wa kimataifa unaoipa Misri haki miliki ya maji ya Mto Nile unaoanzia Ziwa Victoria, alikwenda kwenye mkutano wa maji mjini Cairo, ambako alikutana na mambo mawili makubwa.
"Wakati nateremka pale airport, nilikuta ulinzi wa hali ya juu sana, nikauliza iweje mimi waziri tu nipewe ulinzi namna hii! Mwenyeji wangu akatabasamu tu.
“Siku ya pili yake, nikaenda kwenye mkutano na waandishi wa habari, sijawahi kukutana na idadi kubwa namna ile ya waandishi wa habari, wakati ule wao walikuwa wanamjua Mwalimu Nyerere na timu ya Simba tu ambayo iliwafunga, sasa walitaka kumjua huyo Lowassa ni nani mwenye jeuri na nguvu ya kutaka kutumia maji haya.
“Wakaniuliza, kwa nini nataka kutumia maji yale wakati kuna mkataba unaozuia, nikawaambia, kule Tanzania kuna watu wanakaa umbali wa kilomita tano tu kutoka ziwani, lakini hasa kina mama wanalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 20 kwenda kutafuta maji.
“Baadaye nikawaambia, tutayachota maji yale, mtake msitake, wakashangaa, nikaondoka na sasa mnaona faida ya msimamo wangu," alisema.
Awali, Mgeja aliwapiga vijembe wanasiasa wanaompiga vijembe Lowassa, kwa kusema kuna kikundi cha wanasiasa wahuni wanaomuonea wivu Lowassa.
"Kundi hili lishindwe na lilegee kwa jina la Yesu," alisema Mgeja, huku akishangiliwa na waumini, ambapo alimfananisha Lowassa na mto mkubwa Kkama Ruvu na kwamba hakuna anayeweza kukinga mikono kuzuia kasi ya maji yake.
Katika harambee hiyo, Lowassa alichangisha zaidi ya Sh milioni 220, zikiwamo ahadi na fedha taslimu, japokuwa malengo yalikuwa ni kupata Sh milioni 150.
Post a Comment