Siri ya ushindi wa Francis Cheka dhidi ya mmarekani yafichuka.

Siri ya ushindi wa Francis Cheka dhidi ya mmarekani yafichuka.

SIRI ya ushindi alioupata bondia maarufu nchini, Francis Cheka ‘SMG’ dhidi ya Mmarekani Phil Williams imefichuka baada ya mke wa bondia huyo kutoka Morogoro, Tosha Azenga kutoa la moyoni. 


Akizungumza katika mapokezi ya mumewe mwishoni mwa wiki iliyopita alipowasili mkoani hapa, Tosha alisema mumewe amekuwa akifanya vizuri kutokana na ukweli kwamba kila anapokaribia pambano huwa anamnyima unyumba.
  
“Siri ya mafanikio ya mume wangu ni kufanya mazoezi sana na zaidi ya yote anapokuwa na mchezo huwa simpi tendo la ndoa ambalo ni sumu kali ya mazoezi.
 

“Kwa mfano, gemu la juzi na yule Mmarekani, siku chache kabla sikumpa kabisa tendo la ndoa na yeye anakubaliana na mimi kwani anajua nafanya hivyo kwa nia njema, faida yake mmeiona,” alisema Tosha aliyemzalia Cheka mtoto mmoja wa kiume aitwaye Historia

Ushuhuda wa mwanamke huyo ulipongezwa na baadhi ya wadau hasa wanaojua madhara ya kufanya mazoezi sana kisha kuendekeza ngono kwani ni vitu viwili visivyochanganyika.
“Anachofanya ni sawa, huwezi kuwa unafanya mazoezi ya mpira au ngumi kisha ukitoka hapo unaenda kufanya mapenzi, wanaoendekeza hivyo ndiyo hao unasikia leo kafanya vizuri kesho kavurunda,” alisema Hassan Tolu wa Kihonda.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro aliyekuwepo kwenye mapokezi ya Cheka, Mhe. Saidi Amanzi alimpongeza ‘Mrs Cheka’ kwa uamuzi wake ambao umesababisha bondia huyo apeleke heshima nyumbani.
 
“Tumpongeze kwanza Cheka kwani licha ya yeye kuwa bondia na kuwachapa watu kila kukicha lakini muangalieni mkewe, hana alama yoyoye ya kichapo kwenye uso wake.
 


“Pia nimpongeze mama huyu kwani alidai kwamba mumewe anapokuwa na pambano huwa hamgusi kabisa,” alisema mheshimiwa huyo na kushangiliwa na umati uliofurika kwenye mapokezi hayo.

 
Usiku wa Agosti 30, mwaka huu Cheka aliandika historia kama lilivyo jina la mwanaye kwa kumtwanga kwa pointi bondia Phil Williams kutoka Marekani na kutwaa ubingwa wa dunia unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Dunia uzani wa Super Middle.


Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger