SIMBA SC YAMKANA OKWI, YASEMA ALIKUJA KWA SHIDA ZAKE MWENYEWE DAR, WAO WANATAKA 'HELA' ZA WAARABU TU TAREHE 30

SIMBA SC YAMKANA OKWI, YASEMA ALIKUJA KWA SHIDA ZAKE MWENYEWE DAR, WAO WANATAKA 'HELA' ZA WAARABU TU TAREHE 30

Na Ezekiel Kamwaga,
SIMBA SC imesema kwamba haihusiki na ujio wa mshambuliaji wake wa zamani, Emmanuel Arnold Okwi nchini hivi karibuni na inatambua huyo ni mchezaji halali wa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa sasa.
“Katika siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimeripoti kuhusu uwepo nchini wa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa klabu, Emmanuel Arnold Okwi kutoka nchini Uganda,”.
“Taarifa hizo zimeeleza mambo mbalimbali ikiwamo taarifa kuwa Simba Sports Club ina mawasiliano na mchezaji huyo na alikuja kwa mwaliko wa viongozi wa klabu. Baadhi ya vyombo vimekwenda mbali zaidi na kudai kuwa uongozi wa Simba unamshawishi mchezaji huyo avunje mkataba wake na klabu anayoichezea sasa ya Etoile du Sahel  (ESS) ya Tunisia,”.
Alikuja kwa shida zake; Emmanuel Okwi ni mchezaji halali wa Etoile du Sahel

“Klabu inapenda kuuarifu umma kwamba Simba au kiongozi wake yeyote (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Sekretarieti haijahusika kwa namna yoyote ile na ujio wa mchezaji huyo hapa nchini. Hakukuwepo na mwaliko rasmi au usio rasmi kwa viongozi wa Simba,”.
Simba imesema kwamba taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na uongozi wa Simba ni za upotoshaji na zina lengo la kuharibu heshima na hadhi ambayo uongozi huu umeijenga kitaifa na kimataifa kwenye tasnia ya soka.
Imesema kisheria, Simba haiwezi kumzuia mchezaji huyo kusafiri kwenda nchi yoyote anayotaka kama amefuata sheria zote za uhamiaji kwa kuwa Okwi ana mkataba na timu nyingine na Simba haihusiki na safari zake, matembezi yake au mipango yake ya kimaisha.
Uongozi wa Simba umesema unafahamu kwamba Okwi ni mchezaji halali wa ESS maana wenyewe ndiyo uliomuuza kwa klabu hiyo, hivyo kwa mujibu wa sheria za FIFA, klabu yeyote, ikiwamo Simba SC, haziruhusiwi kufanya mawasiliano na mchezaji huyo au yeyote yule halali wa klabu nyingine bila ruhusa ya klabu yake kama mkataba wa mchezaji husika umebakiza kipindi kinachozidi miezi sita. 
“Hii maana yake ni kwamba uongozi hauwezi kumshawishi mchezaji huyo kujiunga na klabu.
Ikumbukwe kwamba hadi sasa, klabu ya Simba, inaidai klabu ya Etoile du Sahel kiasi cha dola za Marekani 300,000 (laki tatu) ambazo zinapaswa kuwa zimelipwa kabla ya tarehe 30 mwezi huu wa tisa mwaka 2013. Kinyume cha hapo matokeo mengine yataamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya FIFA ambapo makubaliano husika yalisajiliwa,”.
Uongozi wa Simba umeomba vyombo vya habari na watu binafsi waache kutoa taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na klabu au kwamba kuna mipango ya kumshawishi avunje mkataba wake kwani taarifa hizo hazina ukweli wowote.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger