Mkuu wa Mkoa Tanga awataka Wanawake Wilayani Korogwe kuwashitaki Wanaume Walevi
Wanawake Wilayani Korogwe wametakiwa kuwashitaki kwa viongozi waume zao ambao wanazitelekeza familia zao kwa ajili ya ulevi.Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Gallawa wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi wa kijiji cha Mafureta kilichopo Korogwe vijijini ambapo aliwataka wanawake kutowaonea huruma wanaume wenye kasumba ya kuzitelekeza familia zao kwa sababu ya ulevi.
Mhe. Gallawa alionekana kukerwa na maisha duni ya wakazi hao wa mafureta licha ya kuzungukwa na mazingira mazuri ya kilimo na kutaka kujua kulikoni, aliwapasha wananchi hao kuwa ardhi ni mali na kwamba hawakustahili kuwepo kwenye lindi la umaskini.
Hata hivyo idadi kubwa ya watu waliofika kumsikiliza Mkuu huyo wa Mkoa walikuwa katika hali ya ulevi huku watoto waliokuwepo kutokuwa na viatu wala nguo zenye kuleta matumaini ya maisha bora kwa mtanzania jambo lililomchefua sana .
“Akinamama toeni taarifa kwenye vyombo vya sheria kwa wababa wanaouza vyakula na kwenda kulewa pombe ama kuongeza nyumba ndogo huku watoto hawana viatu wala vifaa vya shule” alisema Gallawa.
Kwa upande mwingine aliwataka wananchi kuachana na kilimo cha mazoea ambacho alisema kuwa hakiwezi kuwaletea mabadiliko mazuri ya kimaisha kwa kuwa hakina tija wala muelekeo.
Awali Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Lucas Mweri wakati akijibu hoja ya Mkuu wa Mkoa kuhusu mradi wa kijiji hicho, alieleza kuwa kijiji cha Mafureta ni miongoni mwa vijiji vilivyopata fedha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kwamba zaidi ya tsh, million 300 zilitolewa kuiimarisha.
Mweri alieleza kuwa jumla ya tsh million 300 zilitolewa kwenye skimu ya Mafureta kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu na kuboresha thamani ya zao la mpunga na kwamba watakopeshwa pembejeo kwa kulipa wakati wa mazao pamoja na mkakati wa barabara ya uhakika.
Naye Mbunge wa jimbo la Korogwe vijiji, Stiven Ngonyani (Profesa majimarefu) aliwataka wananchi hao kuchangia mambo ya maendeleo yao badala ya kuchanga fedha kwa ajili ya kuleta waganga wa jadi ambao hatima yake ni kusababisha migogoro na jamii kutengana.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini Bw. Lucas Mweri akijibu hoja ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji kijijini hapo
Umati wa wanakijiji waliofika katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa
Baadhi ya watoto waliofika kwenye mkutano wa hadhara
Post a Comment