PADRI wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Monesmo Magamba amemwagiwa tind
ikali na watu wasiojulikana katika Mtaa wa Mlandege jana jioni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Haji Hana alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba kiongozi huyo wa dini amelazwa katika
Hospitali ya Mnazi Mmoja, akiendelea na matibabu baada ya kujeruhiwa
usoni, kifuani na mikononi.
Hana
alisema kwamba Padri Magamba (60) alikuwa akitokea katika duka la
huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine saa 10.15 jioni na watu
waliommwagia walimtega mlangoni kabla ya kufanya uhalifu huo na kutoweka
kwenye vichochoro vya Mitaa ya Mtendeni na Mchangani.
Alisema
polisi wamestushwa na tukio hilo kwa vile limetanguliwa na matukio
matatu ya kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini na kuwataka wananchi
kutoa ushirikiano wa kufanikisha kuwakamata watu wanaojihusisha na
vitendo hivyo.
“Tumeanza
kufanya uchunguzi ikiwemo kuchukua maelezo ya majeruhi, tungependa
zaidi kupata msaada wa kitaarifa kwa watu walioona na wanaojua mahali
walipo watu wanaofanya vitendo hivyo,” alisema Hana.
Mfanyakazi
wa Duka la Huduma za Mawasiliano ya Mtandao, Rukia Yahya Abass alisema
anamtambua Padri Magamba kama mteja wake wa muda mrefu na huja dukani
hapo nyakati za asubuhi au jioni kwa ajili kupata huduma za mawasiliano.
Rukia alisema ameshtushwa kuona padri huyo baada ya kumaliza kupata huduma na kutoka nje akipiga mayowe ya kujeruhiwa.
“Nimezoea
kumwita father au babu, ni mteja wangu kwa kweli, nilimwona akirudi
tena ndani huku akiomba msaada, watu waliokuwa katika mtandao harakahara
wakammwagia maji, alikuwa akilalamika kwa ukali wa maumivu,” alisema
Rukia akiwa na huzuni.
Alisema
wasamaria wema ndiyo waliomchukua na kumpeleka hospitali. Kabla ya
tukio hilo alilipa gharama za huduma ambazo zilikuwa ni Sh2,000 na
kurudishiwa chenji yake baada ya kutoa noti ya Sh10,000.
Daktari
Jamal Adam ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja
alisema kwamba Padri Magamba amepatiwa huduma ya kwanza na anaonekana
amejeruhiwa usoni, mikononi na kifuani.
“Ni mapema mno kusema ameathirika kwa kiasi gani kutokana na tukio hilo, tunaendelea na juhudi za kumtibu, ”alisema Dk Jamal.
Huu
ni mfululizo wa visa vipatavyo vinne vya kikatili ambavyo vimefanyika
Zanzibar, vikiwalenga watu maalumu katika kipindi cha miezi 10
iliyopita. MWANANCHI
Post a Comment