MNEC AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI

                           

MNEC AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI



MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tanga (MNEC), Kasimu Kisauji, amewataka walezi na wazazi wilayani humo kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa bidii na kuacha kukaa vijiweni, hatua inayochangia kutumia muda mrefu kufikiria vitendo viovu.
Kisauji alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na vijana wa shina la Yebo Yebo, Kata ya Ngamiani Kusini jijini Tanga katika ziara ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga (UVCCM) iliyokuwa na lengo la kuupa uhai umoja huo.
Alisema iwapo vijana watakuwa mstari wa mbele kuwajibika kwa kufanya kazi itawasaidia kuwa na maisha bora ambayo yatawawezesha kuinua familia zao na jamii kwa ujumla, hali ambayo inachangia kuongezeka kwa pato lao.
Alisema vijana wamekuwa wakidanganyika kwa kuambiwa kuwa vijiweni ni sehemu ya kubadilishana mawazo, hatua inayowafanya waonekane kama ombaomba kila wakati.
“Maisha bora lazima yaendane na kufanya kazi na si kukaa vijiweni, vibarazani na kuanza kupiga soga zinazorudisha maendeleo nyuma,” alisema.
Akizungumzia suala la mikopo ya vijana na kina mama inayotolewa na halmashauri, Kisauji aliwataka vijana kuacha kulalamika badala yake wajiunge kwenye vikundi vitakavyowasaidia kuwezeshwa kupata mikopo hiyo.
Aliwataka  madiwani wa halmashauri ya jiji hilo kuhakikisha wanasaidia kina mama na vijana ili waweze kupata mikopo hiyo bila kuwepo usumbufu.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger