POLISI TANGA YAKUSANYA MILIONI 801.

POLISI TANGA YAKUSANYA MILIONI 801.

Na Oscar Assenga, Tanga
 
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga Kitengo cha Usalama barabarani, limeongeza makusanyo yanayotokana na makosa mbalimbali, kutoka Sh milioni 738.2 hadi kufikia Sh milioni 801.8. Ongezeko hilo ni la kuanzia mwaka 2012 na 2013, fedha ambazo zilitokana na makosa mbalimbali ya barabarani, baada ya uimarishwaji wa doria kwenye barabara kuu na za mijini.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tanga, Abdi Isango aliyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alisema fedha hizo zilikusanywa kutokana na makosa 26,178 yaliyopatikana mwaka jana na makosa 24,160 yaliyopatikana mwaka juzi.


Isango alisema makosa mengi yanatokana na ubovu wa matairi, kutokufunga mikanda na uendeshaji mwendo kasi ambao mara nyingi husababisha ajali na kupoteza maisha ya raia wasiokuwa na hatia kwa madereva wanaotumia barabara za Mkoa wa Tanga.

Aidha alisema takwimu za ajali za barabarani zimeonekana kupungua kwa kiasi kidogo, kutoka ajali 98 zilizojitokeza mwaka jana zilizosababisha majeruhi 219 ikiwemo watu 129 kufariki dunia kutokana na ajali hiyo, wakati mwaka juzi zilitokea ajali 98 zilizoua watu 104 ambapo ongezeko hilo ni sawa na vifo 25, ambayo ni sawa na asilimia 24 pamoja na majeruhi 153 ikiwa ni ongezeko la asilimia 66.

Akizungumzia ajali za pikipiki kati ya mwaka 2012-2013, Isango alisema ajali hizo zimepungua kutoka vifo 24 mpaka kufikia vifo 21, ambavyo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.5 ambapo punguzo hilo limetokana na waendesha pikipiki wengi kupata elimu ya usalama barabarani na uimarishaji wa doria kwenye barabara kuu zote mkoani hapa.

Aliwataka wananchi kuacha kuendelea kutoa rushwa, kwa sababu kuendelea kufanya hivyo kunaweza kusababisha ongezeko la ajali za mara kwa mara barabarani, kwani wanapokuwa wakitoa rushwa askari wanashindwa kuwajibika ipasavyo na kuyaacha magari kuendelea na safari zake bila kujali madhara yatakayoweza kuwakuta.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger