CHAUSTA WASHINDWA KUFANYA KAMPENI KALENGA
IKIWA zimebaki takribani siku
kumi ili kufungwa kampeni za kugombea ubunge katika jimbo la Kalenga,
mgombea
wa ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA),
Richard Minja anatarajia kuzindua kampeni kesho katika kijiji cha Wasa
Kata ya Maboga.
Akizungumza na mtandao huu leo
kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa CHAUSTA, Mwaka Mgimwa amesema licha ya kuchelewa
kuanza kampeni watafanya kazi kubwa ili kuhakikisha wanapata ushindi katika
jimbo hilo.
Mgimwa amesema anatoka kwenye
vikao vya Bunge maalum la Katiba linalofanyika mjini Dodoma kwa ajili ya
uzinduzi wa Kampeni hizo ambapo baada ya uzinduzi watahakikisha wanatafanya
kata kwa kata na kijiji kwa kijiji katika muda huo uliobaki.
Tangu kuanza kwa kampeni Februari
19 mwaka huu, Chama hicho kimekuwa kikishindwa kufanya kampeni kwa sababu
zilizoelezwa kuwa Mgombea huyo yupo nje ya mji kwa shughuli za kijamii na
kushindwa kufuata ratiba kama ilivyo.
Hata hivyo katika ratiba chama
hicho kinaonekana kutokuwa na muda mwingi wa kampeni kulinganisha na vyama vya CCM na Chadema
vinavyoonekana kuwa na muda mwingi wa kufanya kampeni.
Kampeni za jimbo la Kalenga
kwa chama cha CHAUSTA zilitarajiwa kuzinduliwa rasmi tangu February
22 katika kijiji cha kibaoni kata ya Ifunda jimboni humo ambapo tangu ratiba
kuanza chama hicho hakijawahi kuonekana kufanya mkutano hata mmoja.
Mtandao huu ulipomtafuta mgombea
huyo kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi zaidi juu ya kukwama kwa kampeni
katika chama chake amesema hangeweza kuzungumza chochete kwa kuwa yupo nje ya
mji.
“Nipeni muda kwa sasa siwezi
kuliongelea hilo suala nitawapeni jibu kesho asubuhi. Kampeni zipo nyingi mimi
ninafanya za kimya kimya sio lazima
nifanye kampeni na matarumbeta, magari na mziki ndio mjue nafanya kampeni
kwasababu kila mtu anatumia staili yake ya kufanya kampeni” amesema Minja.
Hata hivyo alipododoswa zaidi
amesema kuwa kutumia hela nyingi kwenye kampeni ni kuwadanganya wananchi
kwasababu wao ndio wanashida nyingi na wanahitaji msaada kutoka kwa viongozi
hivyo ni bora pesa zitunzwe ili baada ya ushindi zitumike kuwaletea maendeleo
wananchi.
Hata hivyo mgombea huyo ametuma
ujumbe mfupi kuwa bado yuko nje ya mji na anatarajia kurudi leo kwa ajili ya kuandaa shughuli za uzinduzi
wa kesho katika kijiji cha Wasa Kata ya Maboga.
Post a Comment