JK kupokea Rasimu ya Katiba Mpya Jumatatu

JK kupokea Rasimu ya Katiba Mpya Jumatatu

 

Tume  ya Mabadiliko ya Katiba inatarajiwa kuwakabidhi Marais Jakaya Kikwete na Dk Mohamed Shein, rasimu ya katiba mpya.

Hafla ya makabidhiano hayo itafanyika Jumatatu, kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Tume, Assaa Rashid, ilisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kuendelea kuwepo kwa tume hiyo, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki, alisema tume itakabidhi nyaraka hizo na itaendelea na kazi.

Alisema itavunjwa kwa mujibu wa sheria baada ya rasimu hiyo kufikishwa na kusomwa kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Taarifa ya Rashid ilieleza kuwa hafla hiyo pia inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wa kisiasa, taasisi na asasi mbalimbali zikiwamo za kidini na kiraia pamoja na wananchi.

Taarifa hiyo ilisema Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba, anatarajia kuwakabidhi Marais, ripoti ya mchakato pamoja na rasimu ya katiba mpya.

Rasimu hiyo imetokana na maoni ya wananchi, viongozi na makundi mbalimbali waliyoyawasilisha kwa tume kupitia njia mbalimbali zikiwamo mikutano ya hadhara, barua pepe, njia ya posta, tovuti (www.katiba.go.tz) na ukurasa wa facebook wa tume (Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania) na mabaraza ya katiba.

Mchakato wa kupata katiba mpya ulianza Julai, mwaka jana baada ya kuundwa kwa sheria ya kuanzisha tume ya mabadiliko ya katiba.

Kwa mujibu tangazo la Rais Kikwete kuhusu kuandikwa katiba mpya Tanzania inatarajia kuwa na katiba mpya ifikapo Aprili 2014, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Baada ya kuundwa tume hiyo ilipewa miezi 18 ya kutekeleza jukumu la kukusanya maoni, kuyachambua na kutayarisha rasimu ya awali ili ijadiliwe na wananchi na kuandaa toleo hilo linalokabidhiwa kwa maraisi wiki ijayo.

Baada ya kuzunguka Bara na Visiwani Tume ilikusanya maoni kuyachambua na kutoa rasimu mpya iliyutoka  Juni mwaka huu na kujadiliwa kwenye mabaraza ya katiba ili kuiboreshwa zaidi.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na rasimu ya awali ni kuwepo kwa serikali tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Kadhalika ilizungumzia kuwepo kwa wagombea binafsi, kuondoa viti maalumu vya ubunge, kuweka ukomo wa ubunge na kuainisha mambo ya Muungano kuwa saba.

Bunge Maalumu
Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba, baada ya kukabidhi rasimu hiyo ni kuitishwa Bunge Maalumu la Katiba.

Wajumbe wake wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wawakilishi kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 166 watakaochaguliwa na kutoka asasi za kiraia, vyama vya siasa, taasisi za elimu ya juu, wafanyakazi, wakulima na makundi maalumu. 

Bunge hilo litaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni kama Spika ambaye atakuwa na makamu na makatibu. Viongozi hao watachaguliwa kwa misingi ya Bara na Visiwani.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger