Tanga sasa hatarini kupoteza hadhi ya Jiji
Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa
Hayo yalibainishwa jana na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakati wa majumuisho ya ziara yao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajabu Mbaruk, alisema kamati inakwenda kuishauri serikali kushusha hadhi ya kuwa jiji na kurudi katika hadhi ya manispaa kwa kuwa imeshindwa kukusanya mapato.
Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga inatia aibu kwani inakusanya mapato ya Sh. bilioni 3.5 kwa mwaka ambayo ni madogo kulinganisha na ya Jiji la Mwanza ambalo linakusanya Sh. bilioni 10 kwa mwaka.
Alisema cha kusangaza, Halmashauri ya Jiji la Tanga ina vyanzo vingi vya mapato, lakini mapato hayakusanywi na kusema kuwa hiyo ni aibu na haifai kuwa na hadhi ya jiji.
Mbarok alisema kuwa madiwani na watendaji hawana uchungu na halmashauri ya jiji la Tanga. “Sasa kamati inakwenda kuishauri serikali kushusha hadhi jiji la Tanga kuwa manispaa kama zamani,” alisema.
Alisema kuwa Mkoa wa Tanga una wilaya tisa, lakini cha kushangaza ni kuwa mkoa mzima wanakusanya Sh. bilioni nane tu na kuzidiwa na Jiji la Mwanza.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kiasi cha Sh. bilioni mbili za mapato zimepotea kutokana na jiji hilo kutokuwa na uwezo wa kutunza vizuri kumbukumbu za mahesabu.
Alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na lini LAAC itakutana na serikali ili kuwasilisha pendekezo la kulishusha hadhi Jiji la Tanga, alisema kamati yake inaandaa taarifa ya mapendekezo na ili kuipeleka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment