UKATILI WA KIJINSIA:Mume amkata mkewe mkono Kisa: Wivu wa mapenzi

UKATILI WA KIJINSIA:Mume amkata mkewe mkono Kisa: Wivu wa mapenzi

Leah Clement

Majeruhi Leah Clement (24), akiuguza jeraha lake wodini katika Hospitali Teule ya Wilaya Geita kwa madai ya kukatwa mkono wake wa kushoto na mumewe.(PICHA:RENATUS MASUGULIKO)

Mwanamke mkazi wa kijiji cha Nyamikoma Kata ya Bugarama Wilaya ya Geita, Leah Clement (24), anadaiwa kukatwa mkono wake wa kushoto na mumewe kutokana na wivu wa mapenzi.
Hivi sasa mwanamke huyo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita akiendelea kupatiwa matibabu.
Aidha, mtuhumiwa wa ukatili huo, anadaiwa ametoroka na kwenda kujichimbia kwa `sangoma’ kwa imani kwamba hatakamatwa.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 9, mwaka huu saa 1:30  usiku katika kijiji cha Chifufu kata ya Bugarama wilayani Geita.
Imeelezwa kwamba mtuhumiwa huyo alikwenda jikoni kwa mkewe na kukuta akisonga ugali kisha akamvamia na kumshambulia kwa panga lengo likiwa ni kumkata shingo yake.
Hata hivyo, mkewe aliwahi kujikinga shingoni kwa kutumia mkono wake wa kushoto na hivyo kusababisha ukatwe.
Akizungumza akiwa katika wodi alikolazwa majeruhi huyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, aliapa kuwa vitendo vya aina hiyo haviwezi kuvumiliwa katika ya jamii kwani licha ya kuwa vya unyanyasaiji wa kijinsia, pia vinakiuka haki za binadamu na sheria za nchi.
Mangochie ameagiza mtuhumiwa huyo, Mussa Lutobeka (34), akamatwe mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kadhalika, ameagiza mganga wa kienyeji anakodaiwa kukutwa mtuhumiwa amehifadhiwa, pia akamatwe.
Ofisa Mtendaji wa kata ya Bugarama, Juma Choma, alisema walimkamata mtuhumiwa huyo nyumbani kwa mganga wa kienyeji, Mashindeke Mwanzalima (47), akiwa amejificha chini ya uvungu wa kitanda.
Hata hivyo, Choma alisema walipokwenda nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji, alikana kuwapo kwa mtuhumiwa huyo.
Lakini alisema baada ya kumbana na kuipekua nyumba yake, walimkuta mtuhumiwa wa ukatili huo akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda.
“Ndipo nilipoamuru mganga huyo naye akamatwe,” alisema.
Watuhumiwa wote wawili wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Leonard Paul, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na watuhumiwa kukamatwa.
Akizungumzia tukio hilo huku akibubujikwa machozi wodini likolazwa, Leah alisema kabla ya tukio hilo, mumewe ambaye ana wake wawili, alikuwa akimtishia kuwa siku moja atamuua kama hataondoka.
Mke mwingine wa mtuhumiwa huyo anadaiwa alikimbia.
Kutokana na vitisho hivyo, Leah alikwenda kutoa taarifa kwenye ofisi ya kijiji, lakini askari mgambo waliokwenda nyumbani, hawakumkuta mtuhumiwa baada ya kutoroka.
Leah alisema alilazimika kuondoka nyumbani kwa mumewe na kwenda wa baba yake mdogo hadi ufumbuzi utakapopatikana.
Kwa mujibu wa Leah, aliolewa na mume huyo mwaka 2008 akiwa na umri wa miaka 19 baada ya wazazi wake kupokea mahari ya Sh. 400,000 kati ya 500,000  alizokuwa amepangiwa kutoa.
Aidha, alisema wazazi wake (Leah), Clement Jading’wa na Rehema Rehema Kasabuku, walitengaba tangu mwaka 1995.
Leah anasema wakiwa na mume wake, wamebahatika kupata watoto wawili, Happiness Mussa (5) na Merciana Mussa (3).
Hata hivyo, alisema watoto hao kwa sasa wanaishi kwa baba yake mzazi tangu walipofarakana na mumewe.
Daktari wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk. Leah Kusalula, alisema ulemavu alioupata majeruhi huyo, ni wa kudumu na ni kitendo cha ukatili wa kutisha wa kijinsia ambao haupaswi kuvumiliwa.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger