MATOKEO YA AJABU: SIMBA YAPELEKA MAAFA JANGWANI 1977 (4)

MATOKEO YA AJABU: SIMBA YAPELEKA MAAFA JANGWANI 1977 (4)

simba_enzi_zao_3e490.jpg
Wachezaji wa Simba wakiwa 'wameulamba'.

Na Daniel Mbega
KATIKA mchezo wa soka kushinda ama kushindwa ni mambo ya kawaida, lakini vipo vipigo ambavyo timu hupata kiasi cha kujiuliza mara kumi kumi, kulikoni? Kama kuna kipigo ambacho kitabaki katika kumbukumbu za Yanga milele na milele ni kile cha mwaka 1977 cha magoli 6-0 (MNYAMA).
kutoka kwa watani wake wa jadi, Simba, kwenye mchezo wa Ligi ya Taifa.
Kwa waliokuwepo na waliopata simulizi baadaye, Jumanne ya Julai 19, 1977 ilikuwa siku yenye majonzi makubwa kwa mashabiki wa Yanga na furaha kubwa kwa wale wa Simba, ambayo kwa ushindi huo, mbali na kujihakikishia ubingwa wa Ligi ya Taifa kwa kuwa ilibakiza mechi moja tu dhidi ya Navy (sasa KMKM) ya Zanzibar iliyokuwa ya kukamilisha ratiba, pia ilikuwa imefanikiwa baada ya miaka tisa kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-0 na Yanga mwaka 1968.
Kati ya watu waliojihisi wenye furaha kupindukia walikuwa kocha wa Simba, Dimitier Samsarov wa Bulgaria ambaye alikuwa na muda mchache tu tokea akabidhiwe timu na nahodha Abdallah Kibadeni 'Mputa' ambaye siku hiyo 'alicheka' na nyavu mara tatu.
Ilikuwa hadithi ya kifo cha nyani miti yote huteleza, kwani pamoja na kukuru kakara zote za Yanga, ikiwemo kubadilisha wachezaji wawili dhidi ya mmoja wa Simba, ambaye alibadilishwa kufuatia mwenzake kuumia (Martin Kikwa ndiye aliyeumia na kumpisha Abbas Dilunga), mambo yalichacha na kuvunda kwa vijana wa Jangwani waliokuwa wakipokea mashambulizi mfululizo na kubaki wakitumia ujanja wa mtego wa kuotea (offside-trick), ambao hata hivyo, haukusaidia kitu.
Mwaka huo Yanga ilikuwa haijatulia baada ya mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 uliopelekea karibu wachezaji 20 nyota kufukuzwa kwa madai ya kutokuwa wazalendo na kusababisha Yanga kupoteza taji lake la ubingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka huo. Wachezaji hao ni Gibson Sembuli, Leodgar Tenga, Sunday Manara, Boi Idd 'Wickens', Ally Yusuf, na wengineo ambao walikwenda kuunda timu ya Nyota Afrika ya Morogoro kabla ya kuanzisha Pan African ya Dar es Salaam.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger