WAKAZI WA VIJIJI VYA KIDUNDAI, KILUWAI NA VUGA WALILIA BARABARA

WAKAZI WA VIJIJI VYA KIDUNDAI, KILUWAI NA VUGA WALILIA BARABARA

OFISI ya Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Tanga inaombwa kuangalia uwezekano wa kuiingiza kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha barabara ya Mombo- Bangala chini- Kidundai- Kiluwai- Vuga yenye urefu wa km 9 ili kuwapunguzia kero ya usafiri wananchi wa maeneo hayo.

Wanaomba barabara hiyo ya kiwango cha vumbi kwa kuanzaia angalau itengewe fedha za kuifanyia ukarabati maalum utakaohusisha kazi za kuchonga, kupasua miamba (mawe makubwa) na kunyoosha ili kuwapa fursa wanakivijiji wanaoishi mlimani kusafirisha kwa Mpunga na Mahindi ambayo wanayalima katika mashamba yalioko katika skimu ya umwagiliaji ya Mombo.


Baadhi ya wanakijiji waliozungumza katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili alipotembelea vijiji hivyo mwishoni mwa wiki walisema wanashangazwa na hatua ya Tanroads mkoani Tanga kuamua kuitelekeza barabara yake hiyo kwa miaka mingi sasa bila kuifanyia matengenezo yanayostahili.

Wakulima hao walisema utekelezaji wa hatua hiyo utasaidia sana wavijiji wa Kidundai na Kiluwai vilivyopo kata ya Vuga kupunguza gharama wanayoipata sasa ya kulazimika kusafirisha mazao toka shambani kwa umbali wa zaidi ya km. 30 kwa kupitia barabara ya Mombo- Vuga- hadi Kidundai.


Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Kidundai, Mbwana Rashidi alisema kwa sasa barabara hiyo haipitiki kabisa kwa gari kwasababu inazo kona nyingi zenye mawe makubwa ambazo wananchi wameshindwa kuzinyoosha kwa kutumia sururu na majembe.

“Tunao utaratibu wa kufanya kazi za msaragambo kama wanakijiji ambapo katika barabara mara kadhaa tumelazimika kuchimba kwa mikono ili angalau pikipiki na baiskeli ziweze kupita lakini pamoja na jitihada zetu hizo Tanroads na pia halmashauri yetu hapa wilayani hawajawahi kutusaidia kabisa”,alisema na kuongeza.

“Tunajisikia vibaya na tunadhani serikali yetu imetutenga na Tanroads wametutelekeza kwa hiyo hatuna ila tunahitaji vifaa kama baruti za kuweza kulipulia hayo mawe makubwa njiani ndipo tutaweza kuendelea kuchonga kwa mikono baadhi ya maeneo korofi ili tuweze kupata barabara ya kupitisha magari”,alisema.

Alitaja maeneo hayo korofi yenye mawe makubwa kwamba ni yaliyopo vitongoji vya Madudani ukitokea Bangala chini, Kwemgongo, Kwekiseti, Kwemishwihi na Kiluwai shule na kusema maeneo hayo kwa ujumla yana urefu wa km 4.

Mkulima mmoja aliyejitambulisha kama Mohamed Abdala  alisema kwakuwa Kidundaji iko juu mlimani wanalazimika kushuka uwanda wa chini ambako ni Kata ya Mombo iliyoko wilayani Korogwe ili kulima mazao ya Mpunga na Mahindi kila msimu.

“Kwa hali ilivyo sasa baada ya kuvuna na kupakia mazao kwenye malori tunalazimika kupitia barabara yenye urefu wa km 30 kwa gharama ya sh. 100,000 kwa safari badala ya kutumia sh. 40,000 kwa barabara ya Kidundai yenye urefu wa km 9 kutoka mashambani Mombo ….hii ni kero tunaomba serikali itusaidie”,
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger