WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI JIJINI TANGA WATISHIA KUSITISHA HUDUMA

WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI JIJINI TANGA WATISHIA KUSITISHA HUDUMA

Na Oscar Assenga, Tanga.
BAADHI ya wamiliki wa vyombo vinavyotoa huduma ya Usafiri jijini Tanga wametishia kusitisha kuendelea kutoa huduma hiyo kutokana na gharama kubwa wanazozipata wakati wa matengenezo yanayotokana na ubovu wa barabara zilizopo jijini Tanga.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya barabara za jijini Tanga kuwa na mashimo hali ambayo inapelekea kuleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji wake hasa nyakati zinapokuwa zikinyesha mvua.
Mwenyekiti wa Muungano wa wasafirishaji abiria mkoa wa Tanga,(Muwata) Hatwabi Shabani  alisema barabara ambazo zimekuwa kero kubwa sana ni Sahare, Makorora, Mikanjuni, Raskazone mwisho,Japani,Kivumbitifu na Kasera.
Shabani alisema kutokana na ubovu wa njia hizo wamiliki wa magari zinazofanya safari zake katika maeneo hayo wamekuwa wakipata hasara na hivyo kumuomba mkurugenzi wa Jiji la Tanga kuangalia uwezekano wa kuzifanyia matengezo barabara hizo.
Mwenyekiti huyo alisema wao kupitia muungano wao wanaomba maeneo hayo yafanyiwe matengenezo madogo madogo angalau kufukia yale mashimo ambapo magari mengi yanaharibika kitendo ambacho kinapelekea baadhi ya wamiliki kutaka kuhamisha magari kutokana na gharama kubwa za matengenezo.
Aliongeza kuwa wanaiomba Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha wanazifanyia kazi changamoto hizo ili chama hicho kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa Jiji la Tanga.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger