TANROADS TANGA YAPITISHA MAOMBI YA KUPANDISHWA HADHI BARABARA BUMBULI.
(Meneja wa Tanroads mkoa wa Tanga,Mhandisi Alfred Ndumbaro|}
Raisa Said,Tanga.
Bodi ya Barabara Mkoani Tanga (TANROADS)
imepitisha maombi ya kupandishwa hadhi barabara zenye urefu wa kilometa 130
zinazounganisha vijiji 9 katika Halmashauri mpya ya Bumbuli, mkoani Tanga.
Akiwakilisha ombi hilo kwa wajumbe wa
Bodi ya barabara iliyokutana hapa mwishoni mwa juma lilipita, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatrice Musomisi alisema amewasilisha
maombi kwa ajili ya kupandishwa hadhi barabara za halmashauri ya Bumbuli ili
ziweze kuhudumiwa na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS).
Msomisi alisema kwamba barabara hizo
ni muhimu kwani zinaunganisha makao makuu ya Bumbuli na halmashauri za wilaya
ya Lushoto na Korogwe kupitia kwenye barabara za mkoa za Mombo/Lushoto/Soni/Bumbuli/Dindira
na Kwamote pamoja na Mashewa na Bombo Mtoni.
Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya
Bumbuli alizitaja barabara zitakazounganishwa na vijiji 9 kuwa ni
Soni/Mponde/Funta/Tamota/Kerenge ambazo zina urefu wa kilomita 60.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni
pamoja na Mbelei/Mgwashi/Milingano/Mashewa zenye urefu wa kilomita 70.
Hata hivyo, Msomisi alifafanua kuwa
kupandishwa hadhi kwa barabara hizo kutasaidia usafirishaji wa mazao ya
wakulima katika jitahada za kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuinua
maendeleo ya Halmashauri ya Bumbuli kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Meneja wa Tanroads Mkoani
hapa, Eng. Alfred Ndumbaro maombi hayo ya barabara yamefuata taratibu zote
ndani ya Halmashauri ya wilaya na kwamba vikao husika vilikaa na kupitisha
maombi hayo.
Meneja huyo wa barabara alizitaka
halmashauri za wilaya kuzipa umuhimu wa matunzo barabara zote zinazohudumiwa na
Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kuwa ni chanzo cha maendeleo.
Post a Comment