WAZIRI MKUU PINDA AMUONYA VIKALI MAGUFULI


WAZIRI MKUU PINDA AMUONYA VIKALI MAGUFULI




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amemuonya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa mara nyingine tena kuacha tabia ya kufanya uamuzi wa jambo lolote bila kushirikisha pande zinazohusika.

Mbali ya karipio hilo, Waziri Mkuu amewataka viongozi wengine wa Serikali, kuepuka mfumo usio shirikishi katika uamuzi wao kwa kuwa unasababisha migogoro ndani ya jamii na usumbufu kwa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya mgomo wa wasafirishaji wa mizigo na abiria ulioanza Oktoba 5, mwaka huu, Pinda alisema Serikali imeamua kurejesha kwa muda wa mwezi mmoja asilimia tano ya uzito wa mizigo uliozidi kwenye mizani.


Alisema hatua zilizochukuliwa na Dk. Magufuli kufuta vifungu vilivyokuwa vikiruhusu asilimia tano zilifuata sheria, lakini tatizo lililojitokeza ni kutoshirikisha pande zinazohusika ili kushauriana na kupata uamuzi wa pamoja.

Alisema mbali ya kutoshirikisha pande hizo, uamuzi wa Dk. Magufuli ulikuwa wa ghafla kwa wasafirishaji kitendo ambacho kimewapa wakati mgumu wa utekelezaji, kwa sababu wafanyabiashara walikuwa wameingia mikataba na wateja wao.

“Chimbuko la mgogoro huu, ni tangazo la Dk. Magufuli alilotoa Oktoba mosi, mwaka huu la kuondoa ofa ya asilimia ya uzito uliozidi, baada ya uamuzi huo wadau wa usafirishaji wa malori na mabasi waliingia kwenye mgomo na kulalamikia hatua hiyo.

“Kutokana na mgogoro huu, nililazimika kukutana na Dk. Magufuli, baadhi ya mawaziri wa wizara zenye uhusiano na masuala haya, wanasheria na wataalamu wa masuala ya usafiri na uchumi.

“Kilichoongeza mgogoro ni tafsiri ya vifungu vya sheria na kwenye kanuni ya 7 (2) na 7(3) ambacho kinaeleza wasafirishaji wa magari yenye uzito uliozidi, lakini upo ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria, wanatakiwa kupunguza mzigo, kupinga na iwapo watashindwa kutekeleza, watatakiwa kulipia mara nne ya tozo za kawaida.

“Sasa suala la asilimia tano, lilitokana na ombi la wadau wa usafirishaji kwa aliyekuwa waziri wa Ujenzi miaka ya nyuma na halikuwa sheria kamili, ndio maana limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya.


“Nakubaliana na Dk. Magufuli, wapo baadhi ya wasafirishaji ni wakorofi na hawataki kufuata sheria…ndio maana walifanya mazoea ingawa wapo wengine wazuri na hao nawapongeza sana kutii sheria.

-Mtanzania

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger