King Majuto: Njaa, shida za wananchi zinanilazimu nigombee Ubunge Tanga Mjini 2015
Na Kambi Mbwana, Dar es Salam
MSANII wa filamu na vichekesho wa muda mrefu hapa nchini,
Amri Athuman maarufu kama King Majuto, amesema hali ya Tanga ilivyokuwa sasa na
ugumu wa maisha unamlazimisha aingie kwenye siasa kwa ajili ya kuwania Ubunge
mkoani Tanga.
Msanii
wa vichekesho Tanzania, Amri Athuman, maarufu kama King Majuto,
pichanii, aliuhakikishia mtandao huu nia yake ya kuwania Ubunge mwaka
2015 kwa tiketi ya CCM
Majuto anataka kugombea Ubunge katika Jimbo la Tanga mjini, ambapo kwa sasa lipo chini ya Mbunge wake Omar Nundu, jambo linaloanza kuibua maswali kede kede miongoni mwa wadau wa sanaa wanayempenda mzee Majuto.
Mbunge wa Tanga Mjini, Omar Nundu, pichani.
Akizungumza na Handeni Kwetu mapema wiki hii, King Majuto
alisema kwamba atagombea Ubunge kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama
anachokipenda na kukiheshimu kwa kiasi kikubwa mno kutokana na mfumo wake wa
uongozi.
Alisema watu wamekuwa wakiishi maisha magumu na yenye
kukatisha tamaa, hivyo ni wakati wake sasa kuingia katika ulingo huo ili
amalizie wakati wake kwa ajili ya kuwapatia maisha mazuri wananchi wa Tanga na
Tanzania kwa ujumla.
“Kuna watu wanaweza kusema labda njaa ndio inayonifanya
niingie kwenye siasa na kutaka kuwania nafasi kubwa ya Ubunge, ila lazima
wajuwe kuwa sina njaa kwakuwa kazi ninayoifanya inanipa fedha za kutosha na
maisha yangu ni mazuri.
“Nina mpangilio mzuri wa kazi zangu, bado naheshimika kwa
kiasi kikubwa na kazi zangu zinapendwa, ila kuingia kwenye siasa ni kwasababu
nina malengo mazuri na wanananchi wa Tanga Mjini na Tanzania kwa ujumla, hivyo
hakuna wa kunizuia,” alisema Mzee Majuto.
“Kwa sasa nipo sawa zaidi na malengo yangu hayo naoamba
Mungu yafanikiwe bila kuogopa majina ya wanasiasa waliokuwapo au wanaoweza
kupambana na mimi katika nafasi hiyo, tukianza ndani ya CCM na baadaye Uchaguzi
Mkuu,” aliongeza Majuto.
Kauli ya King Majuto inaweza kuleta picha ya kupendeza kwa
wadau wa sanaa Tanzania, huku akiwa ni miongoni mwa wasanii wanaokubalika kwa
kiasi kikubwa mno. Bila shaka kwa kauli hiyo inaongeza ugumu wa siasa za mwaka
2015 huku kila mmoja akiona ana uwezo wa kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa
hapa Tanzania.
Post a Comment