Dk Shein:Hakuna maendeleo bila amani

Dk Shein:Hakuna maendeleo bila amani

baraza_586f6.jpg

Wafuasi wa dini ya Kiislamu jana waliadhimisha Idd El-Haj katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania huku Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akitaka Watanzania wasahau suala la maendeleo bila ya amani na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) likimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukutana na wapinzani.
Akihutubia Baraza la Idd El-Haj jana katika Chuo Kikuu cha Taifa (Suza) kilichoko Mkoa wa Kusini Unguja,Dk Shein alisema mipango ya maendeleo ya nchi haiwezi kufikiwa bila ya kuwapo kwa mazingira ya amani na utulivu.

Alisema vitendo vya hujuma dhidi ya raia vinavyofanyika kwa kutumia tindikali lazima vipigwe vita na wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama nchini. "Inafaa tuelewe kuwa, bila ya amani hatutoyafikia malengo tuliyojiwekea ya kuendeleza ustawi wa nchi yetu na watu wake,"alisema Dk Shein.

Dk Shein alisema kwamba vitendo vya hujuma dhidi ya raia wasiokuwa na hatia vimekuwa vikisababisha hofu kwa wananchi na wageni na vinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu na mafundisho ya Mwenyezi Mungu dhidi ya waja wake.

Aidha alisema watalii wanaotembelea Zanzibar wanavutiwa na ukarimu wa wananchi wake pamoja na hali ya amani na historia ya visiwa vya Zanzibar.

"Tusichezee wala tusidharau amani tuliyonayo badala yake,tuitunze na tuiendeleze kwani inapotoweka inachukua muda mrefu kuirejesha sawa na kujenga nyumba ni kazi kuliko kubomoa,"alisema Dk Shein.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuunganisha nguvu zao kupitia vikundi vya Polisi jamii kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua watu wanaotaka kuchafua sifa ya Zanzibar.
Alisema kazi ya kulinda amani ya nchi ni jukumu la kila mwananchi kuahidi Serikali itaendelea kuwasaka wahusika wa vitendo hivyo na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

Dk Shein alisema kuwa,Serikali itaendelea kutekeleze dira ya Maendeleo ya 2020 pamoja na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini kwa wananchi wake (MKUZA) na tayari ufanisi wa mipango hiyo umeanza kuonekana licha ya kuwapo changamoto.

"Uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 7.0 kutoka 6.7 kwa mwaka 2011 tofauti na ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.3 katika Bara la Afrika,"alisema Dk Shein.

Bakwata wamempongeza Rais Kikwete siku moja baada ya Rais Kikwete kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema,Cuf,NCCR-Mageuzi,TLP na UDP,Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limepongeza hatua hiyo na kuita yenye manufaa kwa taifa.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi,Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila akitoa salamu za Baraza la Idd jana katika Msikiti wa Al Farouk uliopo Makao Makuu ya Baraza hilo, Kinondoni Dar es Salaam,alisema uamuzi wa Rais Kikwete una lengo la kuhakikisha mchakato wa Katiba unaoendelea unamalizika kwa amani.

Naye Mgeni rasmi kwenye baraza hilo, Waziri wa Maji,Profesa Jumanne Maghembe, aliwataka Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini na kuepuka ushabiki wenye lengo la kuhatarisha mustakabali wa amani nchini.

Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Ibrahim Yamola na Pamela Chilongola.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger