Utafiti: Wasio na elimu waongoza kumpenda Rais Jakaya Kikwete
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
- “Asilimia 60 ya waliosoma elimu ya sekondari na kuendelea wanaunga mkono utendaji wa Rais, lakini 40 hawakubaliani na utendaji wake,” ilisema taarifa ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Mei hadi Juni mwaka jana.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya utafiti imebaini
kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wenye elimu ya darasa la saba na wale
wasiosoma, ndiyo wanaokubaliana na utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete.
Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la ‘Namna
Watanzania wanavyouangalia utendaji kazi wa Bunge na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania’ ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Asasi ya
Afrobarometer, inaonyesha kuwa asilimia 77 ya waliokosa elimu ndiyo
wanamuunga mkono Rais Kikwete.
Afrobarometa ni Asasi ya Kimataifa inayojumuisha
taasisi tatu za Institute for Democracy ya Afrika Kusini, Ghana Centre
for Democratic Development ya Ghana na Political Science Department ya
Chuo Kikuu cha Michigan cha Marekani.
Mtafiti Msaidizi wa Afrobarometer, Stephen
Mwombela akisoma ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, alisema asilimia 72 ya wale walioishia darasa la saba ndiyo
wanamuunga mkono Rais.
Wakati asilimia 23 ya watu wasiosoma ndiyo
hawamkubali Rais na asilimia 28 ya wale walioishia darasa la saba, pia
hawaridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo.
Mwombela, hata hivyo, alisema utafiti huo
uliohusisha watu 2,400 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonyesha
kuwa idadi kubwa ya wasomi wa kiwango cha sekondari na kuendelea
wanaunga pia mkono utendaji wa Rais, lakini siyo kwa kiwango cha juu
kama wale ambao hawajasoma.
“Asilimia 60 ya waliosoma elimu ya sekondari na
kuendelea wanaunga mkono utendaji wa Rais, lakini 40 hawakubaliani na
utendaji wake,” ilisema taarifa ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika
kati ya Mei hadi Juni mwaka jana.
Matokeo ya utafiti huo yanatofautiana na yale ya
mwaka 2008, ambayo yalionyesha kuwa wasomi walikuwa wanamuunga mkono
Rais kwa asilimia 92.
Pia katika matokeo ya utafiti huo wa mwaka 2008, ulionyesha kuwa wasiosoma walimuunga mkono kiongozi huyo kwa asilimia 92.
Imani ya wananchi kwa Rais
Ripoti hiyo ilisema pia imani ya wananchi kwa
utendaji wa Rais imeshuka hadi kufikia asilimia 74 kwa mwaka jana,
tofauti na asilimia 94 ya mwaka 2005 wakati aliposhika wadhifa huo.
Post a Comment