Gari la wagonjwa latumika kuiba mafuta

Gari la wagonjwa latumika kuiba mafuta

GARI la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nzera kilichopo Kijiji cha Nzera, Wilaya ya Geita mkoani Geita, limekamatwa likiwa ndani ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) likifanya uhalifu.
Gari hilo ambalo hubeba wagonjwa na kuwapeleka katika Hospitali za Wilaya ya Geita, Sengerema na Bugando jijini Mwanza, lilitolewa miezi michache iliyopita na mgodi huo kama msaada kwa ajili ya kituo hicho cha afya.

19520 5d6b4
Gari hilo ambalo lilikamatwa likiwa limepakia mapipa mawili ya mafuta mali ya mgodi huo, lilipokewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Musukuma ambaye pia ni diwani wa kata hiyo.
Tukio la kukamatwa kwa gari hilo, lilitokea usiku wa kuamkia jana usiku ndani ya jengo kubwa la kuhifadhia mafuta ya kuendeshea mitambo linalotumika kama ghala.

Chanzo cha kuaminika kutoka mgodini hapo kililieleza gazeti hili kuwa, gari hilo Toyota Landcruser lenye namba za usajili T 671 AKW lilikuwa likiendeshwa na Mohamed Bihelo (28) ambaye ni mtumishi wa Idara ya Afya, Geita.
Gari hilo lilikamatwa na walinzi wa mgodi huo waliopata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, ambao wamekuwa wakichukizwa na kitendo hicho kwa muda mrefu sasa.
Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya walinzi kupata taarifa na kujiridhisha kuwa gari hilo ambalo lilitolewa na mgodi huo kutokana na kituo hicho kuwa mbali na mji wa Geita na huduma za afya zimekuwa kero.
"Unajua huu mpango huwa unaratibiwa na baadhi ya watumishi wenzetu wa mgodi wasio waaminifu, ndiyo maana hata hii gari ilikamatiwa ndani ya yadi ikiwa imeshapakia mapipa sita ya dizeli," kilisema chanzo chetu jina tunalo.
Baada ya walinzi wa mgodi huo kufika katika yadi hiyo, waligawanyika kwa kuizingira na wengine kuingia kwa ndani kisha kuwaweka chini ya ulinzi wezi hao wa mafuta waliokuwa wamekodi gari hiyo ya wagonjwa.
Hata hivyo imeelezwa kuwa baadaye walinzi hao walipobandua gundi (stika) iliyokuwa imebandikwa ubavuni mwa gari hiyo waligundua kuwa gari hilo ni la kubeba wagonjwa lililotolewa miezi michache na mgodi wa GGM.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa mgodi huo jina lake tunalo, alikiri kutokea kwa tukio hilo ingawa alikataa jina lake kuandikwa gazetini.
Ofisa habari wa GGM, Tenga Tenga alipopigiwa simu hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi (sms) alijibu yuko katika kikao na kuomba atafutwe baadaye.:CHANZO MTANZANIA.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger