Utapiamlo; tatizo sugu linalotesa wengi Kilindi
Makombo Hatibu akimlisha uji wa lishe mtoto Hatibu Abdallah, kushoto ni mtoto Asha Abdalah hivi karibuni mkoani Tanga
Kwenye duka mojawapo lililopo katika eneo la Mgera wilayani
Kilindi mkoani Tanga, nakutana na mama mwenye mawazo mengi, mkononi
amewapakata watoto wawili ambao wanalia muda wote.
Mmoja wao ana tumbo kubwa na mwingine amepauka
uso, nywele zimelainika kwa kiasi kikubwa.Hali ile ilinishtua na
kunilazimu nimsogelee mama yule ili kujua tatizo gani linalomsumbua yeye
na watoto wake.
Kwa upole alinijibu kwa kuanza kunieleza kuwa
watoto wake wanalia kutokana na njaa na kwamba wanakula mlo mmoja na
nyakati za asubuhi anawalisha viporo
Mama huyo, Mwamvua Bakari anasema watoto wake
wamegundulika kuwa na utapiamlo baada ya Kikundi cha Afya na Lishe, Mama
Mjamzito na Mtoto kilichopo Mgera kumtembelea nyumbani kwake na kubaini
watoto wake wanalo tatizo hilo.
Hayuko peke yake, wapo kinamama na watoto wengi zaidi wenye tatizo kama hilo wilayani Kilindi na Mkoa wa Tanga kwa jumla.
Hata hivyo, serikali kwa kushirikiana na wadau wa
sekta mbalimbali za huduma ya afya, mama na mtoto kupitia Shirika la
World Vision wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa
tatizo hilo linapungua nchini.
Kutokana na jitihada hizo, wameweza kupunguza
idadi kubwa ya watoto wanaokufa kwa utapiamlo nchini kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwanamvua kwa upande wake anaeleza kuwa kuanzia
mwaka 2010 wakati alipojifungua mtoto wake wa kwanza maisha yake
yalikuwa magumu kutokana na umaskini unaoikabili familia yao.
Anasema mume wake amekuwa akitegemea zaidi vibarua
vya kulima ili apate fedha ya kununulia walau kibaba cha unga na wakati
mwingine hulazimika kulala na njaa.
“Tatizo kubwa ni kuwa mimi na mume wangu hatuna
kipato, hivyo nilianza kuwaacha watoto wa miezi tisa nyumbani bila
chakula. Kwa sasa, mmoja ana miaka mitatu na mwingine mitano, wote
nilikuwa nikiwaacha kwa bibi yao nao walikuwa wanakunywa uji asubuhi
hadi jioni tutakaporudi kutoka kwenye mahangaiko,” anasema.
Anaeleza kuwa maisha yao yalipokuwa magumu zaidi,
walilazimika kununua nusu kilo ya unga ambao haukutosha, kiasi kwamba
walikula mlo mmoja kwa siku na kulazimika kuacha kiporo ili watoto
wanapoamka asubuhi waweze kula.
Baada ya kikundi hicho kuwatembelea nyumbani kwao
walimweleza aende kliniki kwa ajili ya kupima uzito wa watoto hao. Mtoto
wa miaka mitatu alikutwa na uzito wa kilo 11.3 na yule mwenye miaka
mitano akiwa nazo kilo 10.3 pia.
Mama mwingine mwenye watoto pacha wenye miaka miwili
aliyejitambulisha kwa jina la Makombo Hatibu anasema watoto wake
aliwaanza kula kiporo cha ugali wakiwa na umri wa miezi sita.
Anasema inategemea siku hiyo kama unga umebaki
kidogo anawapikia uji kama hakuna siku hiyo analazimika kumsubiri mume
wake hadi hapo atakaporudi jioni ili wapike chakula.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Afya ya Lishe, Mama
Mjamzito, Muya Atanasia anasema waliwabaini watoto hao wakati wanapita
nyumba kwa nyumba wakitoa elimu ya lishe.
Anasema baadaye waliwachukua wazazi hao kwa ajili
ya kutoa elimu ya lishe bora ili waweze kujifunza jinsi ya kutengeneza
lishe isiyokuwa na gharama kwa kutumia mazao wanayolima kijijini hapo.
Anaelezea kikundi chao kinawakusanya watoto wote
waliopata utapiamlo kwa kuwapikia uji wa lishe uliochanganywa na
karanga, mchele, ulezi na maharage wakati huo wanawaelekeza wazazi wao
jinsi ya kuandaa vyakula hivyo.
“Baada ya kunywa uji huo tunawapa tunda huku uji
mwingine tunawaelekeza wazazi wao waweke kwenye chupa kama chakula
kimechelewa ili waweze kunywa.
“Kwa kupunguza gharama ya ulezi, mara nyingi
tunawashauri jamii watumie mahindi ya lishe yaliyochanganywa na maziwa
kwa ajili ya kupunguza gharama kulingana na maisha wanayoishi kijijini
huku,”anasema.
Anaongeza kuwa mara nyingi wanaelekezwa kutumia
vipimo zaidi wakati huo wakisisitiza uji huo unapoandaliwa unawekwa
sukari na chumvi wakati wa kuandaa lishe ya watoto hao.
Anaeleza kuwa watoto hawapati muda mzuri wa
kunyonya, hivyo wazazi wao walikuwa hawatambui kuwa viporo kwa mtoto
chini ya umri wa miaka mitano husababisha utapiamlo.
Hawazingatii muda wa kula. Wanakwenda shamba na
wanaporudi jioni ndipo huandaa chakula cha watu wazima na kuwapa watoto
wao bila kujali muda.
“Chakula kikuu wanachopikiwa watoto hao ni ugali
na mlenda na baadaye huwaacha watoto wenyewe wale wenyewe. Kwa mfano
kama watoto hawa wawili pacha tumewakuta katika hali mbaya ,” anasema
mratibu huyo.
Katibu wa kikundi hicho, Mwajabu Mrisho anasema
ndani ya siku saba watoto hao waliongezeka uzito. Yule mwenye miaka
mitano aliyekuwa na kilo 10.3, aliongezeka na kufikia kilo 11.9 huku
mwenye miaka mitatu aliyekuwa na kilo 11.3 hakuongezeka uzito kwa sababu
alikuwa na minyoo pamoja na malaria.
Anasema kwa watoto wale pacha, yule wa kike alikuwa na uzito wa
kilo 6.5 aliongezeka na kufikia kilo 7.1 na yule wa kiume aliyekuwa na
kilo 5.9 aliongezeka na kuwa na kilo 6.8.
Mwajabu anasema wamefanikiwa kutoa elimu ya afya
ya mama mjamzito na mtoto, hivyo kutokana na elimu hiyo wanaume wameanza
kuwasindikiza wake zao hadi vituo vya afya na hata kujaribu
kuwashawishi wake zao kuhudhuria kwenye kliniki mara kwa mara.
Mpango wao kwa mwezi Desemba mwaka huu utatoa
elimu katika vijiji vya Jungu, Makingo, Kwendiswati pamoja na Lekiting’e
ambapo awamu ya kwanza elimu hiyo ilitolewa kwenye vijiji vya Mgera,
Balang’a na Kisangasa na kwamba uhamasishaji utaongezeka.
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kata ya Kibirashi,
Augustino Semzige anasema kupitia mradi huo, umesaidia kupunguza ugonjwa
huo kwa asilimia 75. Miaka ya nyuma uliongezeka kwa asilimia 95 kwa
sababu ilitokea njaa kubwa wilayani hapo.
“Mradi huu wa Afya, Mama na Mtoto iongeze nguvu
kwa suala la utapiamlo, hasa kuielimisha jamii ili waweze kujua jinsi ya
kuandaa lishe ya mama mjamzito na mtoto. Kama mama mjamzito akikosa
virutubisho wakati wa mimba anaweza kupata upungufu wa damu na
kusababisha kuvimba miguu na uso ambapo anakuwa hana nguvu ya kumsukuma
mtoto wakati wa kujifungua,” anasema Dk Semzige
Pia, ushiriki wa wanaume kupitia mradi huo
umesaidia kwa asilimia 95 walioanza kuhudhuria kliniki wakiwa na wake
zao. Hivyo mwanamume anapogundua kuwa mke au mama ana matatizo, anakuwa
mstari wa mbele kumpeleka kwenye kituo cha afya.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Wilayani
Kilindi, Ruth Ligubi anasema zaidi ya wanaume 6,197 wamekuwa
wakishirikiana na wake zao baada ya kupata elimu ya lishe kwa mama
mjamzito na mtoto. Kupitia mradi huo, huwajali familia zao na kuzipa
kipaumbele lishe bora na kumjali mama mjamzito.
“Wanaume waliokuja na wake zao kuanzia Januari
hadi Desemba mwaka 2013 walikuwa 6,197 ukilinganisha na miaka ya nyuma
walipokuwa hawazidi 30. Hivyo kwa sasa uelewa umekuwa mkubwa,” anasema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Dk Shemdaa
Ngereza anasema tatizo la utapiamlo ni kubwa hasa kwenye maeneo ya
vijiji vya ndani kutokana na kipato kidogo cha fedha cha kuandaa lishe.
Anasema asilimia 4.5 ya watoto waliougua
utapiamlo, imepungua kutokana na elimu inayotolewa na mradi wa Afya,
Mama na Mtoto kupitia World Vision.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
Post a Comment