UKATILI:MTOTO ABURUZWA NYUMA YA PIKIPIKI NA BABA YAKE KISA HAJAENDA SHULE
Mtoto Anastazia Jumanne (12) ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya msingi katika wilaya na mkoa wa Geita amefanyiwa
ukatili wa kutisha baada kufungwa mpira kwenye pikipiki na baba yake
mzazi na kisha kuanza kumburuza mtaani.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya sa tatu asubuhi katika moja ya mitaa ya mjini humo ambapo inadaiwa kuwa binti huyo anayesoma darasa la nne katika shule hiyo alikataa kwenda shule kitendo ambacho kilimkasirisha baba yake aitwaye Jumanne Nkoyogi ambaye pia ni mfanyabiashara wa samaki mjini Geita.
mashuhuda wa tukio hilo baada ya kuona asubuhi hiyo mtoto huyo akiburuzwa huku amefungwa kwenye pikipiki walianza kupiga makelele na kukusanyana kwa lengo la kumkamata baba huyo aliyekuwa anafanya unyama huo.
Baada ya kumkamata na kumtia kumtia mikononi mwao walimpeleka kwenye ofisi ya sungusungu iliyopo Ihayabuyaga kata ya Kalangalala na kufungiwa humo kwa usalama wake.
Akizungumzia tukio hilo katibu wa sungusungu kata ya Kalangalala aliyempokea mtuhumiwa huyo Abel Richard amesema tukio hilo liliwafanya wananchi kujaa jazba dhidi ya mzazi huyo na kutaka kumpiga.
Amesema mzazi huyo kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi wilayani Geita baada ya katibu huyo kuwasiliana na uongozi wa jeshi hilo na kuwatuma askari kwake kumchukua haraka kwa usalama wake.
Afisa upelelezi wa mkoa wa Geita Simon Pasua amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi hadi sasa kwa upelelezi zaidi.
Post a Comment