Ashindwa Kwenda Shule Kwa Kukosa Ada
Mwenjuma M. Magalu (kulia) akiwa na Bibi yake nyumbani kwao Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni
Mwanafunzi
Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari
Komnyang’anyo wilayani Handeni akimuonesha mwandishi fomu ya kuitwa
shuleni
Na Joachim Mushi, Handeni
LICHA
ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi wote waliofaulu
darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na kidato
cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule
kutokana na kipato duni cha familia zao.
Mwenjuma
M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo
wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi walioshindwa kujiunga na
sekondari kutokana na mama yake kushindwa kumgharamia mahitaji ya shule.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, wilayani
Handeni, katika utafiti uliofanyika kwa ushirikiano na Chama cha
Wanahabari Wanawake (TAMWA), mama wa mtoto huyo Hadija Magalu
aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu alisema ameshindwa kumsomesha
mwanaye kutokana na kipato duni alichonacho.
Magalu
alisema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu Desemba 12, 2011 na
kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule ulipofika
(Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika
shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.
“Naweza
kukuonesha hata baadhi ya vitu ambayo nilikuwa tayari nimenunua kama
sare, kwanja na mahitaji mengine madogo madogo…aliyenikwamisha na
kunivunja moyo ni babayake (baba wa mtoto), ambaye awali niliwasiliana
naye kupitia kwa ndugu zake na kuahidi angenisaidia ada lakini hakufanya
hivyo hadi muda wa kwenda shule ulipofika,” alisema Magalu.
Mume
wa Magalu (jina tunalo) ametelekeza familia yake (watoto wanne) pamoja
na mkewe kwa zaidi ya miaka minne sasa kwa kisingizio kwamba amekwenda
nje ya Wilaya ya Handeni kutafuta maisha, huku mkewe akibaki akiangaikia
familia hiyo.
“Tumekuwa
tukisikia tu kwamba ameonekana kijiji fulani lakini ukifuatilia
humpati, na mara nyingi anapowasiliana na ndugu zake ndio wanatupa
taarifa zake…nami niliwasiliana naye mara ya mwisho nikimpata taarifa za
mtoto kufaulu lakini hakutekeleza ahadi yoyote juu ya kunisaidia ada ya
mtoto.
Michango
iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga na kidato cha kwanza
ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha ya madawati
15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi sh.
5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh.
2,000.
Akihutubia
Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania lililomalizika hivi karibuni,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara,
Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma na Tanga,
wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na Kidato
cha Kwanza.
Hata
hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa moja ya kampuni
za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha Msasa,
kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha
anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.
Mwandishi
wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Handeni, Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake haina taarifa za mtoto
huyo kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi amueleze
mtoto huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na
ikiwezekana kusaidiwa.
“Kama
huyo mtoto yupo mwelekeze aje pale ofisini kuna wataalamu wa utambuzi
watamuhoji na kuangalia namna ya kumsaidia…sisi hatuna taarifa hizo na
huenda wahusika wanatuficha,” alisema kiongozi huyo.
Post a Comment