Lissu: CCM wana chuki na Warioba
MNADHIMU wa
Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, jana alichafua hali ya
hewa akisema kuwa CCM ina chuki na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Kwa mujibu
wa Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Warioba
na wenzake waliingiza mapendekezo ya serikali tatu kwenye rasimu,
kinyume cha msimamo wa CCM.
Lissu
aliibua tafrani hiyo bungeni jana wakati akichangia hoja ya kuunga mkono
mapendekezo ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, katika muswada wa
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba akitaka mapendekezo ya
serikali ya kuivunja Tume ya Katiba mara baada ya kukabidhi rasimu ya
pili kwa Bunge Maalumu la Katiba yabadilishwe.
Badala yake,
Mnyika alitaka tume hiyo iendelee na kazi hadi Bunge Maalumu la Katiba
litakapomalizika ili kusaidia kutuoa ufafanuzi wa hoja
zitakazojitokeza.
Akichangia hoja hiyo baada ya wabunge kadhaa wa CCM kuwa wameipinga, Lissu alisema anajua kwanini hawataki.
“CCM wana
chuki na tume ndiyo maana wanataka ivunjwe, isiwepo kabisa wakati wa
Bunge Maalumu, sababu ni yule mzee Warioba kuingiza mapendekezo ya
muundo wa serikali tatu ambao hawautaki.
“Kwa hiyo
hawa wanataka wale wajumbe wasiwepo kabisa maana wameingiza mambo
kinyume cha matarajio yao,” alisema Lissu na kuongeza kuwa CCM wamefikia
hata hatua ya kupingana na mwenyekiti wao katika hilo.
Baada ya
Lissu kuketi, Lukuvi alisimama kwa hamaki akiomba kutoa taarifa huku
akijigamba kuwa lazima afichue siri ya jambo hilo ingawa hakutaka
kufanya hivyo.
“Mh. Spika
alichokisema Lissu ni uongo, CCM haijawahi kupendekeza jambo hilo.
Naomba nitoe siri, maana mimi nilikuwa mwenyekiti wa vikao hivyo vya
majadiliano kati ya rais na vyama,” alisema.
Huku wabunge
wakimsikiliza kwa umakini, Waziri Lukuvi alisema pendekezo hilo
lililetwa na CUF kwa maandishi chini ya uwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu
wao (Bara), Julius Mtatiro.
“Nasema siri hiyo ili mjue kuwa hilo ni wazo la CUF mshirika wa CHADEMA wala si la CCM,” alisema.
Wakati
huohuo, Bunge lilikataa pendekezo jingine la Mnyika la kutaka idadi ya
wajumbe wa tume wa kutoka kwenye makundi iongezeke kutoka 166 hadi 292,
tofauti na pendekezo la serikali na kutoka 166 hadi 201.
Muswada huo
ambao ulikuwa na mapendekezo matano ya serikali yaliyofikiwa baada ya
majadiliano kati ya rais na vyama, ulipitishwa kwa pamoja na wabunge
wote wakiuunga mkono.
Post a Comment