Tuhuma nzito bungeni,ni za rushwa dhidi ya Waziri Mkuu Pinda.
Hali
ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel
Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa
waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika
tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk.
Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya
vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa
serikali mbili.
Kauli
hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha
mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa
aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile
baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi hilo walicharuka na kujaribu
kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa iwapo Wenje asingeomba radhi,
asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje,
ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba
wapinzani “walilia” sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa
kutokana na Chama cha Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana
wapatikane wajumbe wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba
walioteuliwa katika kundi hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee
maarufu ambaye ameingizwa kama mganga wa jadi.
Ingawa
hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge
Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.
Kuhusu
rushwa, Wenje alisema:“…Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa
kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi
vilifanyika usiku. Hii haikubaliki.”
Baada
ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe alisimama ghafla huku
akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan
alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa
Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo,
akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni
mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna
kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli
niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini
hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza
kupewa rushwa.
“Kwa
sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo
aniombe radhi. Wenje aniombe radhi,” alisema Profesa Maghembe akiwa
katika hali ya hasira, huku kukiwa na sauti za kuzomea na kushangilia
kutoka kwa wajumbe.
Credit:Mwananchi.
Post a Comment