CHADEMA YATOA UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA NDUGU ALI O. CHITANDA

CHADEMA YATOA UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA NDUGU ALI O. CHITANDA

c1_24e5d.jpg
UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA NDUGU ALI O. CHITANDA
Kutokana na kuwepo kwa taarifa ya Ndugu Ali Omari. Chitanda, huku pia waandishi wa habari wakitaka kujua na kupata ukweli kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA, tunapenda kutoa ufafanuzi mfupi;
Kwanza suala la maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi ndani ya chama, Ndugu Zitto Kabwe na Dkt. Kitila Mkumbo, chama kimeshafunga mjadala kwenye vyombo vya habari kwa kuheshimu na kuzingatia taratibu za kikatiba za ndani ya chama kuendelea.
Pili kuhusu suala la restructuring ya Makao Makuu ya Chama. Chitanda ametoa taarifa akiwataja wakurugenzi wafuatao, kuwa ni wapya;
1.Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson.
2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika
3. Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.

Wakurugenzi wote aliowataja si wapya. Mkurugenzi pekee ambaye uteuzi wake ni mpya na umefanyika hivi karibuni na kuthibitishwa ni Mwanasheria Peter Kibatala, atakayesimamia Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu.
Kama ni suala la kuangalia mtu anatokea wapi (ambalo halijawahi wala haliwezi kuwa moja ya vigezo), ili kuonesha ukweli na kubainisha uongo wa watu wanaojaribu kufanya kazi ya CCM wakisema wao ni wanaCHADEMA, kwa kutumia propaganda zile zile na kuzifanya kuwa ni kete zao za kisiasa ndani ya chama, tunaweza kutaja maeneo ya wanakotoka au asili yao kama ifuatavyo;(P.T)
Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji, Antony Komu- Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare- Kagera.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila- Dodoma.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John John Mnyika- Mwanza
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema- Kilimanjar.o
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala- Morogoro.
Hadi sasa uteuzi wa kurugenzi za Makao Makuu ya CHADEMA haujakamilika. Bado kuna nafasi zinazotakiwa kujazwa kwa kufuata taratibu za chama.
Hii ni kwa sababu maboresho yanayofanyika ndani ya chama, hadi sasa yanaendelea katika ngazi ya Makao Makuu na kanda, kisha itaendelea kwa ngazi za mikoa, wilaya, majimbo, kata, kijiji na hatimaye kitongoji.
Katika maboresho hayo, kwa nafasi za uteuzi, yanayoendelea sasa ambayo yanakwenda hatua kwa hatua, hadi kuwa na makatibu wa kuajiriwa ngazi ya chini ya chama, chama kinazingatia uwezo, uadilifu na utayari wa mtu katika kutoa utumishi bora kwa wanaCHADEMA na Watanzania wote katika nafasi husika.
Suala la maslahi ya watumishi wa CHADEMA ni utaratibu wa chama ambao unajadiliwa, kufikiwa uamuzi na kisha kuridhiwa kwenye vikao vya chama, kama ilivyofanyika kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichoketi karibuni.
Katika suala hili la maslahi ya watumishi wanaojitolea Makao Makuu ya CHADEMA ambayo si siri, Ndugu Chitanda amesema uongo mkubwa. Kusema kwamba Ofisa Mwandamizi anaweza kulipwa posho kubwa kuliko Mkurugenzi wa kurugenzi husika, ni uongo unaovuka mipaka.
Ndugu huyo anadhihirisha uongo huo yeye mwenyewe kwa kuandika hivi; "800,000/= za awali na sasa itakuwa ni kuanzia Tshs. 1,500,000-2,500,000/= kwa Mkurugenzi na kutoka Tshs.6,800,000/= kwa Afisa Mwandamizi na sasa ni Tshs.1,000,000-1,500,000/=".
Pia si kweli kuwa kila mtumishi anayejitolea Makao Makuu analipwa. Mathalani, wakurugenzi wenye nafasi za ubunge, hawalipwi hata shilingi moja kwa kazi zote wanazokitumikia chama na Watanzania kwa ujumla.
Kwa maelezo hayo ya kutengeneza, ni kwamba hadi sasa Ofisa Mwandamizi anapokea posho kubwa kuliko Mkurugenzi na hata baada ya maboresho atapata posho kulingana na Mkurugenzi. Anapaswa kuwa mkweli. Mtu anayetaka kuonekana muungwana, anapaswa kujiweka mbali na uongo pamoja, maneno ya kutunga pamoja na upotoshaji wa makusudi.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, restructuring inaendelea. Ni hatua kwa hatua. Itafika ngazi za chini kama Baraza Kuu lilivyoagiza. Kwa sababu hiyo hadi sasa uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Wilaya haujafanyika.
Hata hivyo ruzuku imekuwa ikipelekwa kila kanda, mkoa, wilaya na jimbo kama ilivyoridhiwa na Kamati Kuu. Na hii ni zaidi ya pikipiki, kompyuta na magari yaliyopelekwa kila kanda. Angelikuwa mkweli, nagelisema na hili pia.
Ndugu Chitanda anajichanganya sana katika taarifa yake yote. Hii ni moja ya sifa ya kukosa hoja hivyo mtu anaamua kuibua viroja au kutunga maneno kwa sababu ya kujaribu kuukana ukweli anaoujua moyoni. Tutatoa mfano mmoja;
Kupitia taarifa yake, anasema alikuwa mtu aliyeaminiwa hadi kuwa katika vikao muhimu, lakini wakati huo huo anasema kuna ubaguzi! Tunapaswa kumhurumia kwa kushindwa kuunganisha hata mawazo yake na kupata mtiririko wa hoja zenye mantiki! Angelikuwa mkweli angesema katika vikao vya sekretarieti na CC, aliingiaje kama kuna ubaguzi wa dini!
Kwa sababu anazozijua yeye, Ndugu Chitanda ameamua kujipachika cheo ambacho hajawahi kuwa nacho. Amejiita kuwa ni Katibu wa Sekretarieti ya Makao Makuu.
Ndani ya CHADEMA pamoja na kwamba nafasi hiyo imetajwa ndani ya Katiba ya Chama, hakuna mtu ambaye ameteuliwa kutumikia nafasi hiyo. Kama anaweza athibitishe kwa kutoa barua ya uteuzi kutoka kwa Katibu Mkuu.
Mahali pengine amejitambulisha kuwa ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu. Ofisi hiyo ina Katibu Mtendaji mmoja ambaye ni Mzee Victor Kimesera, mmoja wa waasisi wa CHADEMA.
Operesheni ya Chama inayoendelea nchi nzima kwenye majimbo 103, si suala la siri wala lengo bovu kama anavyotaka umma uamini.
Ni mwendelezo wa mpango mkakati wa chama kupitia progamu za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), unaotekelezwa kwa hatua mbalimbali na kwa mbinu tofauti tofauti pamoja na dhana ya CHADEMA ni msingi.
Operesheni hiyo ambayo ni mwendelezo wa nyingi za namna hiyo zinazokwenda ngazi za chini kabisa za chama, zikilenga kuimarisha taasisi na mifumo, imeanza wiki hii na ilitangazwa mbele ya waandishi wa habari.
Tungependa kumalizia ufafanuzi huu mfupi kwa kutoa tahadhari kwa umma kuwa makini na matamko ya watu wa namna hii. Maana tunajua kwa uhakika yako mengi ya namna hii yataandaliwa na kutolewa kadri ambavyo Watanzania wanakaribia kuona na kuishi matumaini ya mabadiliko ya kiutawala na mfumo ndani ya nchi yao.
Mathalani katika taarifa yake, Ndugu Ali Chitanda amedhihirisha na kuonesha kuwa ni aina ya watu ambao wanaCHADEMA na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwaangalia kwa macho ya kuhoji na tahadhari ya hali ya juu, anasema hivi;
"Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa Zitto Kabwe na Dkt Kitila Mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda."
Aya hiyo pekee inayotumia lugha wanayotumia mahasimu wa CHADEMA, wakiongozwa na viongozi waaandamizi wa CCM, wanaohangaika kutokana na Watanzania kuwakataa, wakijiandaa kuwaondoa madarakani kwa sababu sera zao zimeshindwa, inatosha kuonesha uhalisia wa yeye mwenyewe (mtoa taarifa) alivyo.
Ni kauli za namna hii (kuwatisha na kutaka kuwatenganisha Watanzania) ambazo zimekuwa zikitumiwa na watawala kama njia pekee ya kutaka kuzuia upepo wa mabadiliko unaovuma nchi nzima, zimekuwa zikiwaunganisha zaidi Watanzania kuiunga mkono CHADEMA bega kwa bega, ili kupata haki na matumaini ya wanyonge, katika mapambano ya awamu ya pili, kuelekea uhuru wa kweli.
Imetolewa leo Novemba 30, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger